Matumizi ya kijeshi duniani yaongezeka kwa kiwango kikubwa
28 Aprili 2025Ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Masuala ya Amani (SIPRI) yenye makao yake nchini Sweden imesema ongezeko la matumizi ya kijeshi limeshuhudiwa zaidi Ulaya na Mashariki ya Kati.
Mtafiti wa Mpango wa Matumizi ya Kijeshi na Uzalishaji wa Silaha katika taasisi ya SIPRI, Xiao Liang, amesema matumizi ya kijeshi yamekuwa yakiongezeka katika nchi zaidi ya 100 duniani hali inayotishia kuchochea mivutano zaidi, huku akionya.
"Ongezeko hili la matumizi ya kijeshi ambalo halijawahi kushuhudiwa, litakuwa na athari kubwa sana kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa sababu ili kufadhili ongezeko hilo kubwa, nchi zitatakiwa kuchukua maamuzi kuhusu bajeti zao," alisema.
Mataifa yote ya Ulaya kasoro Malta yameongeza maradufu matumizi ya kijeshi huku Marekani ikisalia kileleni ambapo matumizi yake ya kijeshi yalifikia dola bilioni 997.