Matokeo ya uchaguzi nchini Ujerumani, mwanzo wa mwisho
28 Septemba 2009Angela Merkel amefanikiwa katika matarajio ya lengo lake, anaweza kuunda serikali ya mseto ya rangi nyeusi na njano. Lakini hii hata hivyo si kutokana na mafanikio yake binafsi, badala yake ni kutokana na hali mbaya ya kuporomoka kwa chama cha SPD. Ndio sababu anafikiria Marc Koch katika maoni yake kuwa Angela Merkel atakuwa kiongozi wa muda wa serikali.
Ushindi wake hauwezi kubadili mkondo. Huu ni mwanzo wa kuelekea mwisho, kwani chama cha Kansela Angela Merkel pamoja na kubakia madarakani kimepata matokeo mabaya kabisa kuwahi kuyashuhudi tangu kuundwa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Huenda Kansela akahitaji miaka miwili au pengine mitatu kurekebisha hali hiyo. Matumaini yaliopo pamoja na hayo si kwa sababu tu sasa wahafidhina wanatamaa ya kuleta mageuzi yaliokwama wakati wa serikali ya mseto na Wasocial democrats, bali chama chake CDU/CSU kiliamua kuunda serikali ya mseto na FDP.
Waliberali wamepata matokeo bora kabisa katika historia yao katika uchaguzi wa Shirikisho. Bila shaka FDP itatarajiwa kuyalipia matokeo hayo yawe ya kivitendo badala ya ahadi za maneno matupu.
Sera yao ya kukabiliana na msukosuko wa fedha na kiuchumi na kuhusiana na kodi, ni mambo yaliowavutia wapiga kura na kuwapa pigo CDU na SPD. Kinachosubiriwa ni kuona kama wapiga kura waliokipa imani hiyo watashuhudia ahadi hizo zikitekelezwa au la.
Vyama vya umma kwa hivyo vimepambana katika uchaguzi, lakini hapakutokea hali ya kuvunjika moyo wapiga kura na kampeni kama safari hii. Walichokua wakitafuta ni mustakbali wa uhakika na wenye kuambatana na hali halisi ilivyo. Muungano wa vyama vikubwa Waahafidhina wa Christian Democrats na Wajamaa Social Democrats ulishindwa kuwapa matumaini katika kipindi cha miaka minne iliopita ya serikali yao ya mseto.
Taifa hili sasa limo katika utaratibu wa vyama vitano bungeni.
Kwa upande mwengine miaka minne ijayo itakua wakati wa kutafakari kwa Steinmeier na SPD, kutokana na umaarufu uliotokeza kwa chama cha mrengo wa shoto Die Linke. Na kwa muungano mpya wa Bibi Angela Merkel kinachosubiriwa ni matokeo, la sivyo pengine kwake na CDU utakua ni mwanzo wa kuelekea mwisho.
Mwandishi: Koch,Marc/ZR/S.Kitojo
Mhariri:M.Abdul-rahman