Mateka 4 wa Israel na wafungwa 200 wa Kipalestina waachiwa
25 Januari 2025Mateka hao ambao wote ni wanawake waliachiwa baada ya kupitishwa kwenye kundi kubwa la umma wa watu kwenye Ukanda wa Gaza. Israel nayo imewaachia huru wafungwa 200 wa Kipalestina iliyokuwa inawashikilia kwenye jela za nchi hiyo.
Mabadilishano hayo ya mateka na wafungwa ni sehemu ya makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa wiki iliyopita kati ya Israel na kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza.
Makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa Jumapili iliyopita yamewezesha kuanza tena kuachiwa mateka wa Israel waliokamatwa na wanamgambo wa Hamas walipoivamia Israel Oktoba 7, 2023 katika shambulizi la kushtukiza lililowaua zaidi ya watu 1,200.
Israel ilijibu shambulizi hilo kwa kuanzisha vita vya kulitokomeza kundi la Hamas vilivyodumu kwa miezi 15 na kusababisha mauaji ya zaidi ya Wapalestina 40,000.
Israel yathibitisha kuachiwa huru mateka na imewapokea
Israel ilithibitisha mapema leo kuwapokea mateka hao wanne baada ya kukabidhiwa hapo kabla kwa wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu.
Hapo kabla makundi makubwa ya watu yalikusanyika kwenye Ukanda wa Gaza na mjini Tel Aviv upande wa Israel kungojea kukabidhiwa kwa mateka hao na mabadilishano wafungwa wa Kipalestina.
Hayo ni mabadilishano ya pili ya wafungwa na mateka tangu kuanza kutekelezwa kwa makubaliano legelege ya kusitisha vita kati ya pande hizo mbili.
Makubaliano hayo yanalenga kufungua njia ya kusitishwa kikamilifu moja ya vita vibaya zaidi na vilivyofanya uharibifu usio na mfano kati ya Israel na kundi la Hamas.
Kwa bahati nzuri, makubaliano hayo hadi sasa yanatekelezwa na hakuna mashambulizi ya anga ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza wala maroketi yanayovurumishwa na kundi la Hamas.
Hali hiyo imewezesha kuongezwa kiwango cha misaada ya kiutu inayoingia kwenye eneo hilo dogo linalokaliwa na Wapalestina.
Watu wakusanyika Tel Aviv kushuhudia kuachiwa huru mateka
Kwenye tukio la leo, televisheni kubwa iliyofungwa katika ya medani mjini Tel Aviv ilikuwa ikionesha sura za wanawake hao wanne wanajeshi waliokuwa wakisubiri kuachiwa huru.
Baadhi kwenye umati wa watu walikuwa wamejifunika bendera za Israel na wengine walikuwa wamebaba mabango yenye picha za mateka.
"Nina shauku kubwa na nimeshusha pumzi," amesema mmoja ya watu walikusanyika mjini Tel Aviv kushuhudia kuachiwa huru kwa mateka hao.
"Ndani ya muda mfupi tu, maisha yao yanakwenda kubadilika, lakini sasa ni kwa usalama na wakiwa upande sahihi." amesema mwanaume huyo aliyejitambulisha kwa majina ya Gili Roman.
Amesema dada yake aliachiwa Novemba mwaka jana katika mabadilishano pekee ya wafungwa na mateka wakati wa utekelezaji usitishaji mapigano ka muda mfupi kati ya Israel na Hamas. Roman amearifu kwamba ndugu yake mwingine aliuawa akiwa bado mikononi mwa watekaji.
Usitishaji wa sasa mapigao ulipoanza kutekelezwa Jumapili iliyopita, mateka watatu wa Israel waliachiwa huru kwa mabadilishano na wafungwa 90 wa Kipalestina, wote wakiwa wanawake na watoto.
Leo Jumamosi, wafungwa 200 wa Kipalestina wanaachiwa huru ikiwemo 120 wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa kufanya mashambulizi ya kutisha dhidi ya raia wa Israel.
Wanajeshi walioachiwa ni kina nani na walitekwa wapi?
Wanajeshi wanne wa Israel walioachiwa leo wametambulishwa kwa majina ya Karina Ariev, 20, Daniella Gilboa, 20, Naama Levy, 20, na Liri Albag, 19, na wote walitekwa nyara Oktoba 7, 2023 wakati wa shambulizi la Hamas.
Walichukuliwa kutoka kambi ya jeshi ya Nahal Oz karibu na mpaka wa Gaza pale wanamgambo wa Kipalestina walipoivamia.
Kwenye kambi hiyo, wanamgambo waliwaua wanajeshi 60 wa Osrael. Mateka wote wanawake kutoka kambi hiyo walikuwa wamepewa jukumu la kushika doria na kufuatilia vitisho kwenye eneo lote la mpaka na Gaza.
Mwanajeshi mwingine mwanamke aliyekamatwa pamoja nao, Agam Berger, 20, hajaachiwa katika awamu ya sasa.
Jeshi la Israel lilitoa taarifa mapema siku ya Jumamosi likisema kwamba maandalizi yalikuwa yamekamilika ya kuwapokea mateka hao wanne. Kwanza wamepelekwa hospitali kufanyikwa uchunguzi wa afya kabla ya kuunana tena na familia zao.
Zoezi la makabidhiano wafungwa lashangiliwa Gaza
Katikati mwa mji wa Gaza, makundi ya watu yalianza kukusanyika mapema Jumamosi asubuhi wakati wanamgambo wa Hamas walipokuwa wakitandaza vizuizi kwenye eneo la kuwakabidhi mateka kwa shirika la Msalaba Mwekundu.
Wanamgambo kadhaa wenye silaha na waliofunika nyuso zao walipita wakiwa ndani ya magari ndani ya mitaa ya mji wa Gata.
Hayo yameelezwa na mmoja waliokuwepo kwenye eneo hilo Radwan Abu Rawiya. Watoto walikimbia sambamba na magari ya wanamgambo huku milio ya risasi ya kusherehekea tukio hilo ikisikika.
"Watu walikuwa wakishangilia na kuwangoja mateka," amesema Radwan alipozungumza kwa njia ya simu na Shirika la Habari la Associated Press.
Baada ya mabadilishano hayo, Israel inatarajiwa kuanza kuondoa vikosi vyake kutoka kwenye ujia wa Netzarim unaoitenganisha Gaza pande mbili.
Hatua hiyo itaruhusu Wapalestina walioamriwa na Israel kuhamia kusini mwa ukanda huo kuanza kurejea kaskazini mwa Gaza kwa mara ya kwnaza tangu kuanza kwa vita.
Wale wanaorejea wataruhisiwa kufanya hivyo kwa miguu huku usafiri wa kutumia magari ukizuiwa kwa sasa hadi katika siku zijazo za utekelezaji makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hata hivyo katika hali ambayo haijafahamika jinsi itakavyoshughulikiwa, Israel imesema itazuia Wapalestina kurejea kaskazini mwa Gaza hadi pale mateka mwingine wa Israel atakapoachiwa huru.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema ni lazima mateka huyo Arbel Yehud ambaye ni raia wa kawaida aachiwe kwa sababu ilikuwa ni sehemu ya makubaliano na Hamas.
Katika taarifa yake kundi la Hamas limesema mateka huyo "yupo hai na mwenye afya njema" lakini haijafahamika iwapo itamwachia huru hivi leo Jumamosi.