Matayarisho ya ziara ya Baba Mtakatifu Ujerumani yamekamilika
14 Agosti 2005Kolon:
Matayarisho ya ulinzi mkali kwa ajili ya ziara ya Baba Mtakatifu Benedikti XVI wakati wa mkutano mkuu wa Vijana utakaoanza siku ya Jumanne nchini Ujerumani yamekamilika. Waziri wa Mambo ya Ndani wa mkoa wa North Rhine-Westphalia, Ingo Wolf, amesema kuwa ameshiriki binafsi katika matayarisho hayo ili kuhakikisha usalama wa Baba Mtakatifu na Wageni wapatao millioni moja kutoka ulimwenguni kote. Polisi zaidi ya 12,000, Wazima moto na Askari kanzu watakuwa kazini ardhini, angani na majini. Baba Mtakatifu anatumaini kuwa mkutano huo mkuu utalifanya Kanisa kuwa jipya barani Ulaya. Akihojiwa na Redio Vatikani amesema kuwa ukristo siyo amri na masharti peke yake. Ametilia mkazo kwa kusema kuwa imani ni zawadi na wala siyo mzigo. Mkutano mkuu wa Vijana utaanza kesho kutwa Jumanne mpaka Jumapili ijayo.