Rwanda yatakiwa kuondoa vikosi vyake Kongo
31 Januari 2025Shinikizo linaongezeka kwa utawala mjini Kigali wakati waasi wa M23 inaonekana wanasonga mbele kuelekea mji mwengine wa Mashariki mwa Kongo wa Bukavu.
Mapigano yameendelea kuripotiwa maeneo mbalimbali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakielekea katika mji wa Bukavu baada ya kuchukua udhibiti kamili wa Goma.
Licha ya mapigano kupungua huko Goma, hali ya kibinaadamu inaarifiwa kuwa mbaya. Uhaba wa chakula na bidhaa muhimu, ugavi wa umeme umevurugika, hakuna maji safi huku kukiwa matatizo pia kwenye mtandao wa intaneti.
Raia wa Goma wamesema wanahitaji msaada kwa kuwa mji wao umekuwa kama meli isiyo na nahodha. Hawa ni Isaac Mastaki na Louise Furaha.
Soma pia:Kiongozi wa DRC asema jeshi lake linapambana vikali dhidi ya mashambulizi ya M23
Hayo yanajiri wakati Kiongozi wa kisiasa wa muungano wa waasi wa Kongo unaolijumuisha kundi la M23 Corneille Nangaa ameapa hapo jana kuwa wapiganaji wake hawatauachia mji wa Goma na kusema wataendelea kusonga mbele zaidi ndani ya ardhi ya Kongo hadi mji mkuu Kinshasa. Hata hivyo bwana Nangaa alisema wako tayari kwa mazungumzo na serikali ya Kongo.
Kwa upande wake rais Felix Tshisekedi wa Kongo alitoa wito wa kufanyika kwa uhamasishaji mkubwa wa kijeshi ili kukabiliana na uasi huo huku akitupilia mbali miito ya kufanya mazungumzo na waasi wa M23.
Katika ujumbe wa video, Waziri wa Ulinzi wa Kongo Guy Kabombo Muadiamvita amesema hakuna mpango wowote unaowezekana wa mazungumzo na M23 akisema watasalia Kongo na kupambana hadi kifo.
Juhudi za kidiplomasia kusaka suluhu
Juhudi za kikanda na kimataifa zinaendelea ili kuutafutia suluhu mzozo huo. Rais Kagame wa Rwanda na Tshisekedi wa DRC walizungumza na Rais wa Angola Joao Lourenco ambaye aliteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa mpatanishi katika mzozo huo, na wote wawili waliafiki kutoa ushirikiano wao.
Wakati huo huo, waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot aliwasili nchini Rwanda jana na kukutana na Rais Paul Kagame baada ya kufanya mazungumzo na Tshisekedi mjini Kinshasa.
Alipoulizwa kuhusu kinachoendelea huko Kongo, Rais wa Marekani Donald Trump alisema mzozo kati ya Kongo na Rwanda ni tatizo kubwa sana lakini akakataa kutoa maoni yake zaidi.
Soma pia:Waasi wa M23 wasema watabakia Goma
Mzozo huu unaweza kuikosesha Rwanda misaada ya mamilioni ya dola kutoka kwa washirika wake wa Magharibi baada ya kuonekana kukaidi miito ya kuondoa wanajeshi wake huko Kongo na kuacha kuwaunga mkono waasi wa M23.
Serikali ya Uingereza imesema inatarajia kutathmini upya msaada wake kwa Rwanda kutokana na kuhusika kwake katika mzozo wa mashariki mwa DRC.
Jumanne wiki hii, Ujerumani ilisitisha mkutano uliopangwa kufanyika na maafisa wa Rwanda mwezi ujao na kusema inajadiliana na wafadhili wengine wa kimataifa kuhusu hatua zaidi zinazoweza kuchukuliwa.