Mataifa yaahidi kusaidiana kupata suluhu ya mzigo wa madeni
2 Julai 2025Zaidi ya mataifa 100 yanayohudhuria kongamano hilo la kimataifa yameahidi kusaidia kupata suluhu ya kile walichokitaja kama "bomu linalosubiri kulipuka" kwa kuzingatia mzigo wa deni unaozidi kuyaelemea mataifa yanayoendelea, ingawa yakijikuta kwenye mgawanyiko kuhusiana na namna watakavyolitekeleza hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliliambia kusanyiko hilo kwamba "mzigo wa madeni unaulemaza ulimwengu unaoendelea,"na kusisitiza nguvu ya pamoja katika kuyasaidia mataifa hayo yenye kipato cha chini kujiondoa kwenye changamoto hiyo.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, deni la nje la nchi masikini zaidi limeongezeka zaidi ya mara tatu katika kipindi cha miaka 15.
Mataifa yanayoendelea kwa sasa yanalazimika kuwalipa wakopeshaji dola trilioni 1.4 kila mwaka kulingana na masharti ya mkopo, kiwango kilichoongezeka sana katika miaka 20. Mataifa ya masikini pia yanakabiliwa na mzigo wa riba ambao ni mara mbili zaidi ya mataifa tajiri.
Kulingana na ripoti iliyoagizwa na hayati Papa Francis na kuratibiwa na mwanauchumi na mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Nobel Joseph Stiglitz, zaidi ya watu bilioni tatu wanaishi katika nchi ambazo hulipa fedha nyingi kwenye riba kuliko zinazoingizwa kwenye sekta ya afya
Uhispania yaahidi kupeleka dola bilioni 1.9 IMF
Katika hatua nyingine, Uhispania imeahidi kupeleka nyongeza ya dola bilioni 1.9 katika Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, kama sehemu ya juhudi za kuzisaidia nchi zinazoendelea.
Waziri wa Uchumi Carlos Cuerpo aliiambia Reuters pembezoni mwa kongamano hilo jana Jumanne kuwa Uhispania itaendelea kuwa mfano katika mchakato wa kupata suluhu kwa kutoa sehemu ya fedha kwa maslahi ya mataifa yanayoendelea.
Hatua hii ya Uhispania inalingana na juhudi pana za wafadhili za kusaidia nchi zenye mahitaji, na hasa baada ya Marekani aliyekuwa mfadhili mkuu kukataa kuunga mkono mpango kazi uliofikiwa kwenye mkutano wa kilele wa mwaka jana.
Kwenye kongamano hilo linalofanyika Seville, nchini Uhispania, viongozi kadhaa wa dunia kutoka barani Afrika ikiwa ni pamoja na Rais wa Kenya William Ruto na Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, walitoa wito wa mageuzi kwenye mfumo wa fedha wa kimataifa ili kutatua changamoto ya mzunguko huo mbaya wa kifedha.
Waraka uliopitishwa na washiriki unataka kupitishwa kwa vifungu vya mikopo vitakavyoruhusu nchi zinazokopa kusimamisha kwa muda kurejesha mikopo kutokana na athari za kama maafa ya asili.