Mataifa ya Ulaya: Mpango wa kusitisha vita gaza urejeshwe
22 Machi 2025Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa mataifa ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wametoa mwito wa kurejea mara moja kwenye mpango wa usitishwaji wa mapigano yanayoendelea katika ukanda wa Gaza.
Katika taarifa ya pamoja iliyochapishwa na tovuti ya serikali ya Uingereza mawaziri hao wameeleza kwamba kurejea kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza kumerudisha nyuma matumaini ya watu wa Gaza, mateka wanaoshikiliwa na watu wa ukanda huo mzima.
Soma zaidi. Israel yadungua maroketi matatu yaliyorushwa kutoka Lebanon
Kauli hiyo ya pamoja inakuja siku moja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz kutishia kwamba vikosi vyao vitayapoka maeneo zaidi ya Ukanda wa Gaza na kuwaamuru watu katika ukanda huo kuondoka. Lengo likiwa ni kuweka shinikizo zaidi kwa kundi la wapiganaji wa Hamas kuwaachilia mateka inaowashikilia.
Siku ya Jumanne, Israel ilianza kuishambulia Gaza na kusambaratisha makubaliano ya kusitisha vita yaliyokuwepo tangu mwezi Januari. Hadi sasa zaidi ya watu 500 wameuawa kutokana na mashambulizi hayo kwa mujibu wa mamlaka ya afya Gaza inayosimamiwa na Hamas.