Mataifa ya magharibi ´yakabwa koo´ athari za plastiki
4 Agosti 2025Hayo yameshuhudiwa katika mazungumzo yanayoendelea mjini Geneva kuhusu mkataba wa kimataifa wa
Ingawa mataifa hayo yanajiweka mstari wa mbele kuunga mkono mkataba wenye malengo makubwa, wachambuzi wa mazingira wanasema mchango wao halisi katika uzalishaji wa plastiki hauendani na kauli zao za kisera.
Aleksandar Rankovic, mwanzilishi wa taasisi ya Common Initiative inayofuatilia masuala ya rasilimali za pamoja, amesema haifai kuilaumu tu miungano ya mataifa yanayozalisha mafuta na plastiki kama Saudi Arabia, Urusi na Iran, bila kuangalia jukumu la mataifa tajiri.
"Wote wanadai kuwa na malengo kabambe. Kwangu mimi hilo ni jambo la kinafiki,” alisema Rankovic, akitaja kwamba mataifa ya Ulaya yenye viwanda vikubwa vya plastiki yanapaswa pia kubeba lawama.
Takwimu zinakirejesha kidole kwa mataifa kadhaa za Ulaya
Takwimu zinaonyesha kuwa Ujerumani huzalisha zaidi ya tani milioni nane za plastiki kila mwaka — kiwango kikubwa zaidi barani Ulaya, ikifuatiwa na Ubelgiji na Ufaransa. Kwa pamoja, nchi hizi tatu zinahesabika miongoni mwa wazalishaji wakuu wa plastiki duniani, na bado zinajinasibu kama vinara wa mabadiliko ya kijani.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa matumizi ya plastiki kwa kila mtu barani Ulaya na Amerika Kaskazini yako juu zaidi duniani, yakifikia kati ya kilo 85 hadi 94 kwa mwaka kwa kila mtu.
Kwa kulinganisha, raia wa China hutumia kilo 58 kwa mwaka, licha ya taifa hilo kuwa mzalishaji mkubwa wa plastiki duniani.
Ingawa mataifa ya Magharibi yamejiunga katika kundi linalojiita High Ambition Coalition, Rankovic anakosoa kwamba kundi hilo halijaweka bayana lengo maalum la kupunguza uzalishaji wa plastiki.
Badala yake, linatumia maneno yasiyo na mashiko kama "kupunguza matumizi na uzalishaji wa plastiki hadi kiwango endelevu”, kauli ambayo anaitaja kuwa ya jumla na isiyo na mwelekeo wa utekelezaji.
Ujerumani yajitetea kwamba takwimu zaidi zinahitajika
Katika kujibu lawama hizo, baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mazingira ya Ujerumani wanasema kuwa bado hakuna data madhubuti za kuwezesha kuwekwa kwa lengo la moja kwa moja, kama ilivyo kwa makubaliano ya tabianchi la nyuzi 1.5°C.
Kwa sasa, wanasema, malengo kama hayo hayawezi kueleweka kwa njia ya kihesabu, hali inayotatiza uwekaji wa viwango vya kimataifa.
Hata hivyo, wataalamu wa mazingira wanapinga hoja hiyo, wakisema utafiti wa kisayansi tayari unaonyesha kuwa ni lazima uzalishaji wa plastiki duniani upunguzwe kwa kiwango cha kati ya asilimia 12 hadi 19 ili kufikia malengo ya mkataba wa Paris kuhusu tabianchi.
Serikali ya Ujerumani, kwa kushirikiana na nchi kama Italia, Hispania na Ufaransa, imesema inaunga mkono mpango wa kupunguza uzalishaji wa plastiki ya msingi, kwa lengo la kufunga mzunguko wa matumizi na kuimarisha uchumi wa mzunguko (circular economy).
Hata hivyo, wachambuzi kama Rankovic wanasema hatua hizo bado hazijafikia kiwango kinachohitajika kwa mabadiliko ya kweli.