Mataifa ya Kiislamu yaridhia mpango wa kuijenga upya Gaza
8 Machi 2025Uamuzi wa jumuiya hiyo yenye mataifa 57 wanachama umefikiwa na kutangazwa wakati wa mkutano wa dharura uloitishwa mjini Jeddah, Saudi Arabia, siku tatu baada ya nchi za kiarabu kuuidhinisha mpango huo kwenye mkutano wao uliofanyika nchini Misri.
Kwenye mkutano wa Misri, nchi za kiarabu zilitangaza kuanzisha fuko la kuchangia fedha za kuujenga upya Ukanda wa Gaza.
Mpango huo unalenga kulipiga kumbo pendekezo tata la Rais Donald Trump wa Marekani la kutaka kuichukua Gaza na kuwahamisha waakazi wake wanaokaribia milioni 2. Pendekezo hilo la Trump lilizusha ukosoaji mkubwa kutoka nchi za kiarabu na mataifa mengine duniani.
Hata hivyo mpango ulioridhiwa na nchi za kiarabu na zile za kiislamu haujaainisha nafasi ya kundi la Hamas ambalo Israel inapambana kulitokomeza na inapinga lisihusike kuitawala Gaza baada ya vita kumalizika.