Mataifa ya Kiarabu yasaka namna ya kumkabili Trump
22 Februari 2025Mkutano huo umeangazia pendekezo la Misri la ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita chini ya "usimamizi kamili" wa nchi za Kiarabu. Mvutano umekuwa ukiongezeka baada ya pendekezo lenye utata la Rais Donald Trump wa Marekani la "kuichukua" Gaza na kuwahamishia wakazi wake milioni 2 kwenye mataifa jirani ya Kiarabu.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio ameitetea mipango hiyo ya Trump, akisema haiwezekani kulijenga eneo kama hilo ambalo watu wanaishi chini ya vifusi, lakini pia ambako wanamgambo wa Hamas wanaendeleza shughuli zao. Alisema hayo kwenye mahojiano na mwandishi wa habari Catherine Herridge yaliyochapishwa kwenye mtandao wa X Alhamisi.
Rubioakatoa wito kwa washirika wa kikanda kuja na "mpango bora" ikiwa hawakubaliani na pendekezo la Trump, ambalo lilipingwa vikali na Misri, Jordan na mataifa mengine yenye nguvu ya kikanda, ambalo wanaliona kuwa sawa na ukiukwaji wa mamlaka ya Palestina.
Kujibu hilo, Misri imeendeleza mipango yake ya kuizuia Marekani na Israel kuendeleza ajenda hiyo ya Trump.
Maswali mengi bado hayajajibiwa wakati wa kujadili mustakabali wa Gaza, ikijumuisha, juu ya ni nani hasa anayepaswa kulidhibiti eneo hilo katika siku za usoni, lakini pia kuhakikisha usalama wake.
Soma pia: Al Sisi na Mfalme Abdullah wajadili ujenzi mpya wa Gaza
Israel sio tu inapinga Hamas kuendelea kulitawala eneo hilo bali pia haitaki Mamlaka ya Palestina kuidhibiti Gaza.
Majadiliano yamejikita kwenye ufadhili wa Gaza
Mkutano huo ulioitishwa na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman, umehudhuriwa na Mfalme Abdullah wa Jordan na Mwana Mfalme Hussein, Amiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan pamoja na mshauri wake wa usalama, Emir wa Kuwait Sheikh Meshal al-Ahmad al-Sabah na Mwanamfalme wa Bahrain Salman bin Hamad Al-Khalifa.
Vyanzo vinavyofahamu mazungumzo hayo vililiambia shirika la habari la Reuters kwamba viongozi hao waliliangazia pendekezo la Misri ambalo huena kukahitajika hadi dola bilioni 20 za ufadhili kwa zaidi ya miaka mitatu kutoka kwa mataifa tajiri ya Ghuba na Kiarabu, ingawa hayakutoa uthibitisho rasmi.
Kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa, ujenzi wa Gaza unaweza kugharimu karibu dola bilioni 53.
Kunatarajiwa kufanyika mkutano mwingine wa dharura Machi 4, utakaoandaliwa na Misri, hatua ambayo pia imekaribishwa na mataifa hayo.
Washirika wakuu wa Marekani Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambayo ni mojawapo ya mataifa machache ya Kiarabu kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel, aidha yamepuuzilia mbali mpango huo wa Trump wa kuwahamisha Wapalestina wa Gaza.
Wapalestina na wengine katika eneo hilo wana wasiwasi kuhusu mpango huo kwamba unaweza kuondoa utulivu wa kikanda na pengine kushuhudiwa "Janga ama Nakba" kama iliyoshuhudiwa mwaka 1948 wakati taifa la Israel lilipozaliwa.
Karibu Wapalestina 800,000 walikimbia au kulazimishwa kuondoka kwenye makazi na vijiji vyao. Wengi walilazimika kuishi kwenye makambi ya wakimbizi huko Jordan, Lebanon, Syria, Gaza, Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Israel.