Mataifa 50 yasaka mazungumzo na Marekani ya ushuru wa Trump
7 Aprili 2025Ushuru mpya uliotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump umesababisha zaidi ya nchi 50 kutafuta mazungumzo na Washington. Mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Uchumi Kevin Hassett ameiambia televisheni ya Marekani ya ABC kwamba "zaidi ya nchi 50" zimewasiliana na Ikulu ya White House kuanza mazungumzo ya biashara.
Kauli sawa na hizo zimetolewa na Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent aliyezungumza na televisheni ya Marekani ya NBC. Hassett alisisitiza kuwa ushuru huo hautasababisha kupanda kwa bei za bidhaa nchini Marekani.
Aidha alikanusha kuwa Trump alitarajia ushuru huo mpya utatikisa masoko ya fedha ili kuishinikiza Benki Kuu kupunguza viwango vya riba. Alisisitiza kuwa hakutakuwa na "shurutisho la kisiasa" la benki kuu ya Marekani. Hisa za Marekani zilishuka kwa karibu 10% siku ya Alhamisi na Ijumaa, baada ya Trump kutangaza awamu mpya ya ushuru wa kimataifa.