Mashujaa wa Kiutu wanaosaidia wagonjwa nchini Rwanda
21 Agosti 2025Kuna wakati mtu anaugua magonjwa sugu na ambayo yanamlazimisha kulazwa hospitalini kwa muda mrefu. Lakini huwa ni changamoto kubwa kwa walewasio na uwezo hata wa kupata mlo wa siku. Nchini Rwanda kampuni ya Solid Afrika imeamua kuwasaidia watu kama hawa kwa kuwapa chakula bure wagonjwa wote wasio na uwezo na ambao wamelazwa hospitalini.
Hali hii ilikuwa ikiwaathiri wengi hasa ikizingatiwa kuwa mgonjwa kwa kawaida huhitaji aina mahsusi ya chakula kumsaidia kupata nguvu. Hata hivyo kampuni ya solidi Afrika ambayo hufanya kazi kama wasamaria wema imeleta mapinduzi kuhusu suala hili kwa kujitolea kuwapikia na kuwapa chakula wagonjwa wakiwa hospitali bila malipo. Mukamazimpaka Donatha na Emmanuel Robert ni wauguzi katika hospitali kuu ya Kigali.
Donatha amesema "Kabla ya kuanza mpango huu wa kupelekea wagonjwa chakula mahospitalini, niliwahi kumuuguza mwanangu hapa, haikuwa rahisi kwetu sisi tuliotoka mikoani kupata msaada wa chakula hapa Kigali wakati hauna pesa ya kukusaidia na usimpate wa kukusaidia, lakini sasa kila mtu asiye na uwezo anakuja akiwa na amani moyoni akijua fika kwamba tatizo la chakula halipo tena”
Kampuni ya Solid Afrika kwa sasa imepanua huduma zake hadi katika hospitali kubwa nchini Rwanda na katika hospitali kuu ya Kigali wamejenga jiko kubwa ambalo sasa chakula chao wanaandalia hapo.
Wizara ya afya ya Rwanda inasema inautambua mchango wa kampuni ya Solid Africa kwa uhai wa wananchi na iko tayari siku zote kusaidia kampuni hii kutoa huduma zaidi kwa wagonjwa wengine wenye mahitaji ya namna hii. Iyakaremye Zacharee mfanyakazi wa Wizara ya Afya anasema.
Katika hospitali kuu ya Kigali kwa mfano hadi wagonjwa elfu 8 wanapata msaada wa chakula kila siku kutokana na mchango wa kampuni wa Solid Africa.