Mashirika zaidi ya 100 ya kimataifa yalaani hali ya Gaza
23 Julai 2025Tamko lililosainiwa siku ya Jumatano (Julai 23) na mashirika 111, yakiwemo Madaktari Wasio Mipaka, Save the Children na Oxfam, lilionya kwamba hata wafanyakazi wa mashirika hayo walioko Gaza wanaendelea kufa mmoja baada ya mwengine kutokana na njaa ama kuuawa na wanajeshi wa Israel.
Mashirika hayoyalitowa wito wa kufikiwa haraka "makubaliano ya kusitisha mapigano, kufungua njia zote za kufikisha misaada" na kuiwacha mifumo ya Umoja wa Mataifa kusimamia misaada badala ya shirika la GHF, ambalo yalisema "limethibitisha jinsi lisivyozingatia vigezo vya kibinaadamu kwenye ugawaji wake misaada."
Umoja wa Mataifa unasema vikosi vya Israel vimeshawaua zaidi ya Wapalestina 1,000 waliokuwa wanajaribu kupata msaada wa chakula tangu shirika la GHF, linaloungwa mkono na Marekani na Israel, kuanza operesheni zake mwishoni mwa mwezi Mei.
Witkoff aelekea Ulaya
Kwa upande mwengine, Marekani, ambayo ndiyo muungaji mkono mkubwa wa Israel, imesema mjumbe wake, Steve Witkoff, anafanya ziara barani Ulaya wiki hii kwa mazungumzo juu ya Gaza na huenda pia akaelekea Mashariki ya Kati baada ya hapo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani, Tammy Bruce, aliwaambia waandishi wa habari kuwa "Witkoff anakuja Ulaya akiwa na matumaini ya kupatikana kwa makubaliano mengine ya kusitisha mapigano na pia kuanzisha njia ya kufikisha misaada ya kibinaadamu."
Ziara hii ya Witkoff inafanyika ikiwa ni siku chache baada ya mataifa kadhaa ya Ulaya, zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Denmark, kuungana na mataifa mengine zaidi ya 20 ya Magharibi kuitaka Israel kusitisha mara moja bila ya masharti yoyote vita vyake dhidi ya Gaza.
Shinikizo limeongezekahata nchini Ujerumani, huku wanasiasa na wanaharakati wakiishinikiza serikali mjini Berlin kuchukuwa hatua kali dhidi ya mateso yanayotendwa na Israel kwa watu wa Gaza.
Hali ya Gaza yazidi kuwa mbaya
Ndani ya Gaza kwenyewe hali inazidi kuwa mbaya. Mkuu wa hospitali kubwa kabisa ya ukanda huo amesema kwamba watoto 21 wamekufa kutokana na utapiamlo na njaa ndani ya kipindi cha siku tatu zilizopita.
Usiku wa kuamkia Jumatano, jeshi la Israel liliwauwa watu wengine 21, zaidi ya nusu wakiwa wanawake na watoto, kwa mujibu wa mamlaka za afya katika Ukanda huo.
Jeshi la Israel, ambalo limezidisha makali ya operesheni yake ndani ya mji wa Gaza, lilidai kuwa limewauwa wanamgambo kadhaa wa Hamas katika eneo la Jabaliya.
Jeshi hilop lilisema kuwa ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita lilikuwa limefanya mashambulizi kulenga shabaha 120 "za kigaidi" kote kwenye Ukanda huo.