Gaza: Wito watolewa GHF ivunjwe, yatajwa kuwa mtego wa kifo
1 Julai 2025Zaidi ya mashirika 170 ya misaada ya kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali, yakiwemo Oxfam, Save the Children na Amnesty International, yametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mfumo wa usambazaji misaada unaoungwa mkono na Israel na Marekani huko Ukanda wa Gaza.
Mashirika haya yameelezea masikitiko yao juu ya ongezeko la vifo na vurugu dhidi ya raia wa Kipalestina wanaojaribu kupata msaada, wakisema mfumo huo unakiuka misingi ya kibinadamu.
Katika tukio la hivi karibuni, watu wasiopungua saba wameuawa Jumanne katika maeneo ya kugawiwa misaada. Tukio hilo linakuja siku moja baada ya mashambulizi mabaya ya anga na risasi za moja kwa moja za Israel kuwaua angalau Wapalestina 74, wakiwemo 30 waliouawa kwenye mgahawa wa ufukweni Gaza City na 23 waliopigwa risasi walipokuwa wakitafuta msaada wa chakula.
Shirika la Gaza Humanitarian Foundation (GHF), lililoanzishwa mwezi Mei kwa ushirikiano wa Marekani na Israel, limeshutumiwa kwa kuunda vizuizi vinavyowalazimu raia kukusanyika katika vituo vya misaada vilivyoko chini ya ulinzi mzito — hali ambayo imegeuka kuwa tishio la maisha.
Trump, Netanyahu kujadili mwisho wa vita Gaza
Wakati hali ya kibinadamu ikizidi kuzorota, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anajiandaa kusafiri wiki ijayo kwenda Washington kwa mazungumzo na Rais Donald Trump na maafisa wengine waandamizi wa Marekani.
Mazungumzo hayo yanatarajiwa kugusia mzozo wa Gaza na mustakabali wa vita hivyo. Trump tayari amedokeza nia yake ya kuona mapigano kati ya Israel na Hamas yakifikia mwisho. Aidha, Netanyahu atazungumzia pia mkataba wa kibiashara kati ya Israel na Marekani.
"Mambo haya yanakuja kufuatia ushindi mkubwa tulioupata katika Operesheni ya ‘Simba Anayeinuka' dhidi ya Iran. Kutumia ushindi ipasavyo ni jambo la muhimu sawa na kuupata ushindi wenyewe,” alisema Netanyahu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya Wapalestina 56,000 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa vita hivyo mnamo Oktoba 7, 2023 — shambulio la Hamas lililosababisha vifo vya watu 1,200 nchini Israel na mateka 251 kuchukuliwa. Takriban watu 50 bado wanashikiliwa mateka hadi leo, wengi wao wakihofiwa kuwa wamefariki dunia.
Miongoni mwa matukio yanayoibua hasira ni pamoja na shambulio lililolenga shule ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) iliyokuwa ikihifadhi raia waliokimbia makazi yao.
Wapalestina 500 wapoteza maisha vituo vya GHF
Ingawa halikusababisha majeruhi, liliacha uharibifu mkubwa. Katika maeneo ya Khan Younis na Gaza Kati, maelfu ya watu bado hukusanyika kila siku karibu na vituo vya GHF kutafuta chakula, licha ya hatari.
GHF, ambayo haifanyi kazi chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, inasambaza misaada kupitia vituo vinne vinavyolindwa na walinzi wa kibinafsi.
Israel imekuwa ikisisitiza kwamba mfumo huo mpya unadhibiti matumizi ya misaada ambayo walidai ilikuwa inapokonywa na Hamas — madai ambayo mashirika ya misaada na Umoja wa Mataifa wameyakanusha.
Takwimu za Gaza zinaonyesha kuwa zaidi ya Wapalestina 500 wameuawa karibu na vituo vya GHF katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Ripoti ya UN yataja makampuni yanayowezesha vita Gaza
Katika hatua nyingine inayoongeza presha ya kimataifa dhidi ya Israel, ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyowasilishwa na Francesca Albanese imetaja zaidi ya kampuni 60 zinazodaiwa kufaidika na vita vya Gaza na ujenzi wa makazi ya walowezi.
Kampuni kubwa za teknolojia kama Alphabet, Amazon, na Microsoft, pamoja na watengenezaji silaha kama Lockheed Martin, zimetajwa kwa kusaidia operesheni za kijeshi na ujasusi, ilizozitaja kama kampeni ya "mauaji ya kimbari."
"Wakati maisha katika Ukanda wa gaza yanaangamizwa na Ukingo wa Magharibi ukiwa chini ya mashambulizi yanayozidi, ripoti hii inaonyesha kwa nini mauaji ya kimbari ya Israel yanaendelea: kwa sababu yana faida kwa wengi," aliandika Albanese katika waraka huo wenye kurasa 27.
Aliyatuhumu mashirika hayo kwa kufadhili mipango ya ubaguzi na utengano ya Israel pamoja na kijeshi.
Ujumbe wa Israel mjini Geneva umesema ripoti hiyo "haikuwa na msingi wa kisheria, ni kashfa na matumizi mabaya ya ofisi yake." Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel na wizara ya mambo ya nje hazikupatikana mara moja kutoa msimamo kuhusu ripoti hiyo.
Hospitali ya Al-Shifa yasitisha matibabu kwa wagonjwa wa figo
Kwa upande wa huduma za afya, hospitali kubwa zaidi Gaza — Al-Shifa — imesitisha huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo kutokana na uhaba wa mafuta ya kuendesha jenereta. Wizara ya Afya ya Gaza imetoa onyo kuwa bila mafuta, wagonjwa wengi waliolazwa hospitalini watakabiliwa na kifo.
Katika muktadha huo huo wa maumivu ya raia, familia moja ya watu saba imezikwa Jumanne mjini Zawaida, Gaza Kati, baada ya kuuawa katika shambulio la anga usiku wa kuamkia Jumatatu.
Tukio hilo linaendelea kuwa ukumbusho wa wazi kuwa licha ya wito wa kimataifa wa usitishaji mapigano, mateso na maafa kwa raia wa Gaza bado hayaonyeshi dalili ya kukoma.
Chanzo: Mashirika