Sheria za Israel zayapa hofu mashirika ya misaada Palestina
17 Machi 2025Afisa wa ngazi ya juu wa moja ya mashirika ya misaada ya kiutu ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema hali imezidi kuwa ngumu kwa mashirika hayo baada ya chombo cha Israel kinachofuatilia masuala ya Palestina COGAT kuwasilisha mpango wa kuratibu upya misaada.
Kulingana na mashirika hayo ya hisani, chombo hicho kiliwasilisha mpango unaolenga kuimarisha usimamizi wa Israel wa misaada kwa kuanzisha vituo vya ugavi vinavyohusishwa na jeshi na kuongeza udhibiti mkali wa usambazaji wa misaada ya kiutu. Chombo hicho chenyewe kinasema madhumuni yake ni kukabiliana na uporaji na matumizi mabaya ya misaada ili isiangukie mikononi mwa makundi ya wanamgambo.
Soma zaidi: Mashirika ya UN yasema Gaza yahitaji msaada zaidi wa dharura
Malalamiko hayo yametolewa wakati Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini akikiri kwamba kazi ya kuliongoza shirika hilo si rahisi lakini anaamini kuwa yuko upande sahihi wa historia.
Ameyasema hayo wakati wa mahojiano na shirika la habari la AFP huku UNRWA ikiandamwa na shutuma kadhaa na ukosoaji kutoka kwa serikali ya Israel tangu kundi la Hamas lilipofanya mashambulizi kusini mwa nchi hiyo Oktoba 7, 2023.
Waandamanaji wapinga Netanyahu kutaka kumtimua mkuu wa Shin Bet
Katika hatua nyingine, waandamanaji na ndugu wa mateka wanaoshikiliwa na kundi la Hamas, wameikosoa hatua ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ya kutaka kumfukuza mkuu wa Shirika la ujasusi la ndani Shin Bet, Ronen Bar.
Mmoja wa waandamanaji hao Amit Kalderon amelalamika akisema, "Ronen Bar alikuwa mmoja wa wakuu wa usuluhishi waliokuwa wakijadiliana kuhusu kuwaachilia mateka. Alimtimua kwenye jukumu hilo ingawa ndiye aliyefanikisha makubaliano ya sasa yaliyofanikisha kuachiliwa kwa makumi ya mateka. Na hii ni hatua nyingine kali inayoashiria Israel haina tena demokrasia. Hii ni vita dhidi ya mateka. Ni vita dhidi ya kila Muisrael, Na tutapambana kuipinga."
Jana Jumapili Netanyahu alisema kuwa amepoteza imani na mkuu huyo wa Shin Bet ambaye majukumu yake ni pamoja na kupambana na ugaidi na ulinzi wa maafisa wa serikali hasa wakati mgumu wa vita.