Mashirika ya habari yaitaka Israel kuwaruhusu kuingia Gaza
24 Julai 2025Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa Alhamisi, mashirika hayo ya habari yamesema yana wasiwasi mkubwa kwa ajili ya waandishi wao walioko Gaza, ambao wanazidi kushindwa kujilisha wenyewe na familia zao. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waandishi wanakabiliwa na ukosefu wa mahitaji ya msingi na magumu yanayoendelea katika maeneo ya vita, na wana wasiwasi mkubwa kwamba kitisho cha njaa sasa ni mojawapo ya changamoto zinazowakabili.
Mashirika hayo ya habari yamewasihi viongozi wa Israel kuwaruhusu waandishi hao kuingia na kutoka Gaza, na kwamba ni muhimu chakula cha kutosha kiwafikie watu wa huko. Kutokana na Gaza kuzingirwa, mashirika mengi ya habari ulimwenguni kote yanategemea picha, video na ripoti kuhusu mzozo huo zinazotolewa na waandishi habari wa Kipalestina kwa mashirika ya habari ya kimataifa kama vile AFP.
Idadi ndogo ya waandishi habari wameingia Gaza tangu 2023
Tangu kuzuka kwa vita Oktoba, 2023, idadi ndogo ya waandishi habari wamefanikiwa kuingia Gaza kwa ruhusa tu jeshi la Israel na chini ya sheria kali za udhibiti wa kijeshi. Mwanzoni mwa mwezi Julai, Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka, RSF lilisema kwamba zaidi ya waandishi habari 200 wameuawa Gaza tangu vita vilipozuka.
Huku hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya umesema Israel imefanya juhudi za kuboresha utoaji misaada ya kiutu kwa wakaazi wa Gaza, ingawa hali bado ni mbaya. Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, amesema Alhamisi kuwa kwa sasa umoja huo unatathmini hali hiyo na kwamba mapendekezo yote bado yako mezani, ikiwa Israel haitotekeleza makubaliano yaliyofikiwa na umoja huo mapema mwezi huu wa Julai, kuhusu kuimarisha hali ya kiutu Gaza.
Makubaliano hayo yanajumuisha kuongeza kila siku idadi kubwa ya malori ya chakula na bidhaa zisizo za chakula kuingia Gaza, kufunguliwa kwa vivuko kadhaa katika maeneo ya kusini, na kufunguliwa tena njia za misaada za Jordan na Misri.
Ama kwa upande mwingine Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, ameilaani serikali ya Israel kwa kile alichokiita ''uhalifu wa kivita'' dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi, na Jerusalem Mashariki, na ametoa wito wa uingiliaji kati wa haraka wa kimataifa, ili kuzuia njaa Gaza.
Abbas asema uhalifu hauwezi kuvumiliwa
''Ninasikitishwa na mateso wanayopitia watu wetu wa Gaza, kutokana na kuzingirwa, njaa, na kukosa mahitaji ya msingi zaidi ya maisha. Kinachotokea Gaza ni uhalifu ambao hauwezi kuvumiliwa,'' alisisitiza Abbas.
Wakati huo huo, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, imesema kuwa imeitaka timu yake ya mazungumzo ya Gaza kwenda Israel kwa mashauriano, siku moja baada ya Hamas kuwasilisha majibu kuhusu pendekezo la makubaliano ya kusitisha vita kwa wajumbe wa upatanishi.
Hata hivyo, chanzo kikuu cha Hamas kimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba bado kuna matumaini ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, lakini itachukua siku chache kwa sababu ya kile ilichokiita mkwamo wa Israel.
(AFP, DPA, AP, Reuters)