Israel yatafuta njia kuwawezesha Wapalestina kuondoka Gaza
6 Februari 2025Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameliagiza jeshi la Israel kuandaa mpango utakaoruhusu Wapalestina kuondoka Gaza, kufuatia matamshi tata ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu kuchukua udhibiti wa eneo hilo.
Jumanne, Trump aliushangaza ulimwengu aliposema katika mkutano wa waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu: "Marekani itachukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza na tutaufanyia kazi nzuri. Tutaumiliki."
Alhamisi, Katz aliunga mkono mpango wa Trump, akiutaja kuwa "jasiri."
"Wakazi wa Gaza wanapaswa kupewa uhuru wa kuondoka na kuhamia nchi nyingine, kama ilivyo desturi duniani," alisema Katz. "Nimeagiza [jeshi] kuandaa mpango utakaoruhusu yeyote anayetaka kuondoka Gaza kufanya hivyo, kuelekea nchi yoyote itakayowapokea."
Soma pia: Mataifa yalaani pendekezo la Trump kuwahamisha Wapalestina Ukanda wa Gaza
Katz aliongeza kupitia taarifa kwenye X kwamba mpango wake utawaruhusu Wapalestina kuondoka Gaza "kupitia mipaka ya ardhi, pamoja na mipango maalum ya kuondoka kwa njia ya bahari na anga."
Aidha, alisema kuwa nchi zilizopinga operesheni za kijeshi za Israel Gaza zinapaswa kuwapokea Wapalestina wanaoondoka kwenye eneo hilo.
"Nchi kama Uhispania, Ireland, Norway, na nyinginezo, ambazo zimeitupia Israel lawama na madai ya uongo kuhusu hatua zake Gaza, zina wajibu wa kisheria kuruhusu kila mkazi wa Gaza kuingia kwenye maeneo yao," alisema Katz.
Uhispania yatupilia mbali wazo la Katz
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, José Manuel Albares, alikataa haraka pendekezo hilo.
Wakati huohuo, Netanyahu amepongeza matamshi ya Trump, akiyataja kuwa "wazo la kwanza zuri ambalo nimelisikia," katika mahojiano na Fox News.
"Ni wazo la kipekee, na nadhani linapaswa kuchunguzwa kwa kina, kufuatiliwa na kutekelezwa, kwa sababu naamini litaunda mustakabali tofauti kwa kila mtu," alisema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel alisisitiza kuwa haamini Trump alipendekeza kupeleka wanajeshi wa Marekani kupambana na Hamas Gaza, wala kwamba Marekani itagharamia ujenzi upya wa Ukanda huo.
Soma pia: Pendekezo la Trump kuichukuwa Gaza lakabiliwa na upinzani mkali
Matamshi ya Trump yalisababisha mshtuko kimataifa, huku viongozi kadhaa wa dunia wakiyapinga vikali. Pia, mataifa ya Kiarabu, yakiwemo Saudi Arabia, yaliyataja kuwa hayakubaliki.
Iran, Chaina zakemea juhudi za 'kuangamiza kabisa taifa la Palestina'
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilikataa mpango wa Trump wa kuchukua udhibiti wa Gaza na "kuwahamisha kwa nguvu" wakazi wake wa Kipalestina, ikitoa tamko hilo siku ya Alhamisi.
Msemaji wa wizara hiyo, Esmail Bagahei, alisema kuwa Tehran inaona mpango huo kuwa mwendelezo wa "mpango mahususi wa Israel wa kuangamiza kabisa taifa la Kipalestina," akisisitiza kuwa pendekezo hilo "linakataliwa na kulaaniwa vikali."
Baqaei aliuelezea mpango wa Trump kama "shambulio lisilo kifani dhidi ya misingi ya sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa."
Aidha, alizitaka jumuiya za kimataifa kutambua haki ya Wapalestina ya kujitawala na kuwapatia uhuru kutoka "ukaliaji wa kimabavu na ubaguzi wa rangi."
China pia imeeleza upinzani wake dhidi ya mpango wa kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina wanaoishi Gaza.
"Gaza ni ya Wapalestina, si turufu ya kisiasa, wala haitakiwi kuwa shabaha ya sheria ya msituni," alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Guo Jiakun, katika mkutano wa kawaida na waandishi wa habari.
Aliongeza kuwa Beijing inaunga mkono kwa uthabiti haki halali za kitaifa za watu wa Palestina.