Mashambulizi yaendelea Gaza wakati misaada ikitolewa
28 Julai 2025Mamlaka za Gaza zimearifu kuwa watu 34 wameuawa kufuatia mashambulizi ya Israel, siku moja baada ya kutangazwa hatua ya kusitisha mapigano kwa muda wa saa 10 kwa siku kuanzia saa nne asubuhi hadi mbili usiku katika maeneo matatu ya Gaza city, Deir al-Balah na Mawasi na pia kulegeza vikwazo vya usambazaji wa misaada kutokana na kuzorota kwa hali ya kibinadamu.
Israel haijazungumzia chochote juu ya mashambulizi hayo mapya ambayo yamefanyika nje ya maeneo kulikotangazwa usitishwaji wa muda wa mapigano, lakini imesema kuwa operesheni yake ya kuitokomeza Hamas bado inaendelea katika Ukanda wa Gaza.
Mashirika ya misaada yamepongeza hatua za Israel kuruhusu usambazaji zaidi wa misaada ya kibinaadamu lakini yanasema kuwa hatua hizo hazitoshi ukilinganisha na mahitaji makubwa yaliyopo kwa sasa huko Gaza. Picha za watoto waliodhoofika kiafya zimezua ghadhabu kote ulimwenguni huku idadi ya Wapalestina zaidi ya milioni mbili huko Gaza wakiwa wanategemea misaada ikiwa ni pamoja na chakula.
Juhudi za kidiplomasia zaendelea
Rais wa Marekani Donald Trump atakutana huko Scotland na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na wanatarajia kuujadili mzozo wa Gaza. Trump amesema hakubaliani kabisa na kauli ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliyedai mapema leo kwamba hakuna baa la njaa huko Gaza na kwamba Marekani itachukua hatua kurekebisha hali hiyo.
"Tutaanzisha vituo vya usambazaji wa chakula ambapo watu wataweza kutembea na kuvifikia bila vizuizi. Hakutokuwa na uzio. Watu wanakiona chakula kikiwa mita 30 lakini hawawezi kukifikia kwa sababu kuna uzio uliowekwa ili kuwazuia. Ni mambo ya ajabu yanayoendelea huko."
Kwa upande wake, Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi amemtolea wito Trump kusaidia kumaliza vita vya Gaza akisema kuwa yeye ndiye anayeweza kuvisimamisha vita hivyo, kuwezesha usambazaji wa misaada na kukomesha mateso ya Wapalestina.
Ama Saudi Arabia imesema kikao cha siku mbili kitakachoanza leo katika Baraza la Umoja wa Mataifa ili kujadili suluhisho la mataifa mawili ya Israel na Palestina, ni fursa muhimu ya kukomesha vurugu. Kikao hicho ambacho Saudia itaongoza na Ufaransa kinawelata pamoja maafisa wa ngazi za juu kulijadili suala hilo linaloweza kusaidia kuumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati lakini Israel na Marekani tayari wametangaza kuwa hawatohudhuria.
(Vyanzo: AP, Reuters, DPA, AFP)