Mashambulizi ya Marekani huko Yemen yaua watu 31
16 Machi 2025Mashambulizi ya kwanza ya Marekani dhidi wapiganaji wa Kihouthi wa Yemen tangu kuingia madarakani kwa rais Donald Trump mwezi Januari yamewaua watu 31. Kundi la waasi hao limesema katika ripoti iliyotolewa hii leo.
Msemaji wa wizara ya afya ya serikali ya Wahouthi, Anis Al-Asbahi amesema mashambulizi hayo yamefanyika katika mji mkuu wa Sanaa pamoja na maeneo ya Saada, Al Bayda na Radaa. Watu 31 wameuawa na kuwajeruhi wengine zaidi ya 100, wengi wao wakiwa watoto na wanawake.
Soma zaidi. Rais wa China akataa mwaliko wa EU
Kupitia chapisho lake katika mitandao ya kijamii, Rais Donald Trump wa Marekani ameapa kutumia nguvu kupambana na waasi hao huku akiitolea mwito Iran kusitisha uungaji wake mkono kwa kundi hilo.
Iran kupitia waziri wake wa mambo ya nje Abbas Araghchi imelaani mashambulizi hayo na kusema kwamba Marekani haina mamlaka ya kulazimisha sera zake za nje.