Mashambulizi ya Israel yawauwa watu 60 Gaza
20 Mei 2025Haya ni kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Palestina. Qatar imesema mashambulizi hayo ya Israel yanahujumu juhudi za amani kupatikana katika Ukanda wa Gaza.
Mashambulizi hayo yamefanywa katika nyumba mbili ambapo wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouwawa huku shule hiyo iliyoshambuliwa ikiwa makao ya familia zilizoachwa bila makao.
Jeshi la Israel halikutoa tamko lolote kuhusiana na shambulizi hilo ila hapo Jumatatu liliwatahadharisha wakaazi wa mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza kwamba waondoke katika eneo hilo na waelekee maeneo ya pwani, kwani inajiandaa kufanya "shambulizi kubwa."
Israel itachukua udhibiti kamili wa Gaza
Madaktari wa Gaza wanasema mashambulizi hayo ya usiku wakuamkia leo yamefanywa katika mji a Khan Younis na maeneo ya kaskazini ikiwemo Deir al-Balah, Nuseirat, Jabalia na Gaza City.
Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani, amesema juhudi za amani zimehujumiwa na mashambulizi hayo baada ya kuachiwa kwa mateka raia wa Marekani na Israel Edan Alexander huku kukiwa na operesheni zilizotanuliwa huko Palestina.
Matamshi hayo ya waziri mkuu wa Qatar yanakuja siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kusema kwamba nchi yake "itachukua udhibiti" wa Gaza nzima. Qatar imekuwa mpatanishi mkuu katika vita vya Gaza pamoja na Misri na Marekani.
Mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 500 katika siku nane zilizopita wakati ambapo kampeni hiyo ya kijeshi ikiwa imepamba moto. Hapo Jumanne, jeshi la Israel lilisema liliyakubalia malori matano ya misaada kuingia Gaza baada ya zaidi ya miezi miwili ya kuzuiwa kwa misaada ya chakula na bidhaa zengine muhimu kuingia katika ukanda huo.
Kwa muda sasa Umoja wa Mataifa umesema Gaza, iliyo na idadi ya watu milioni 2.3 inahitaji angalau malori 500 ya malori ya misaada na bidhaa za kibiashara kila siku. Lakini katika kipindi chote cha vita, malori ya misaada yamekuwa yakisubiri katika eneo la mpaka wa Gaza kwa wiki hata miezi wakati mwengine, kabla kuingia.
Israel kuwekewa vikwazo
Haya yanafanyika wakati ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikiwa Wakimbizi wa Palestina UNRWA limesema kuwa kiwango cha utapiamlo kimeongezeka katika kipindi cha wiki 11 ambapo israel imezuia misaada kuingia Gaza.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema aliamua kuingiza misaada hiyo michache baada ya shinikizo kutoka kwa wandani wake, ambao hawawezi kuiunga tena mkono Israel kwa kuwa picha za watu wanaotaabika kwa njaa zinazotokea Gaza.
Ukosoaji wa Israel umeendelea huku Canada, Ufaransa na Uingereza zikitishia kuiwekea nchi hiyo vikwazo na kuitaka kusitisha mashambulizi yake ya kijeshi huko Gaza.
Netanyahu lakini alipuuza ukosoaji huo akisema Hamas wanalipa sasa kutokana na shambulizi lao la Oktoba 7.
Vyanzo: AFP/AP/Reuters