Mashambulizi ya Israel yaua watu 50 Gaza
25 Aprili 2025Mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza siku ya Alhamisi yamewaua watu 50 wengi wao wakiwa wanawake na watoto, Wizara ya Afya ya eneo hilo imesema.
Mashambulizi hayo yameharibu pia makaazi ya watu, kituo chapolisi na hema la kujihifadhi la watu wasio na makaazi. Shambulizi lililofanyika kaskazini mwa Gaza limewaua takriban watu 18 na lingine likiua watu 11.
Soma zaidi: Wapalestina huenda wakateua makamu wa rais kumsaidia Abbas aliyezeeka
Jeshi la Israel limesema limefanya shambulizi katika kituo cha polisi kumlenga mwanamgambo wa Hamas. Katika hatua nyingine jeshi hilo limeripoti pia kutokea kwa kifo cha mwanajeshi wake mmoja huko Gaza wakati wa mapigano.
Mwezi mmoja uliopita Israel ilianzisha upya mashambulizi yake huko Gaza baada ya kuyasambaratisha makubaliano ya usitishaji wa vita baina yake na Hamas huku ikisitisha uingiizwaji wa misaada ya kiutu kuingia Gaza.