Mashambulizi ya Israel yaua 56 Gaza
26 Juni 2025Hayo yanaelezwa wakati ambapo waokoaji katika eneo hilo la Gaza lililokumbwa na vita la Palestina wakisema vikosi vya Israel vimewaua watu 56.
Baada ya zaidi ya miezi 20 ya mzozo mbaya, mashirika ya haki za binadamu yanasema wakaazi wa Gaza zaidi ya milioni mbili wanakabiliwa na hali mithili ya njaa. Israel ilianza kuruhusu usambazaji mahitaji muhimu kuingia katika eneo hilo mwishoni mwa Mei baada ya kuwepo kwa kizuizi kwa zaidi ya miezi miwili, lakini usambazaji wake unaelezwa kutawaliwa na matukio ya fujo na ripoti za karibu kila siku za vikosi vya Israeli kuwafyatulia risasi wale wanaosubiri kuchukua mgao wao.
Israel inafanya mashambulizi zaidi Gaza
Wakati huo huo Israel inaongeza juhudi zake za kulishambulia kwa mabomu eneo hilo la Palestina, katika mashambulizi ya kijeshi ambayo inasema yanalenga kuwashinda wanamgambo wa Hamas ambao shambulio lao la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel lilisababisha vita hivi vinavyoendelea sasa.
Waziri Mkuu wa Uhispania Sanchez mapema leo amesema Gazaiko katika kile amekitaja kuwa "hali mbaya ya mauaji ya halaiki" na ameutaka Umoja wa Ulaya kusitisha mara moja mpango wake wa ushirikiano na Israel. "Nadhani ni dhahiri kabisa kwamba Israel inakiuka ibara ya pili ya mkataba wa ushirikiano, na kwa hivyo nitakachotetea leo katika Baraza la Ulaya ni kwamba Ulaya lazima isitishe Makubaliano ya Ushirikiano na Israel, na kufanya hivyo mara moja."
Kauli hiyo ya Sanchez inaonekana kuwa kali zaidi kuwahi kutolewa, na kiongozi mkuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, hasa akitumia maneno "mauaji ya halaiki" kuelezea hali ya Gaza. Akizungumza kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, kiongozi huyo aliigusia ripoti ya hivi karibuni ya haki za binadamu ya huduma ya kidiplomasia ya Umoja wa Ulaya ambayo ilionesha viashiria kwamba Israel inakiuka wajibu wake wa haki za binadamu chini ya makubaliano ya ushirikiano, ambayo ni msingi wa uhusiano wa kibiashara.
Matumaini ya Trump kumalizika vita vya Gaza
Itakumbukwa Jumatano, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuna hatua zimepigwa katika kumaliza vita vya Israel na Hamas, huku akinukuliwa na waandishi wa habari akisema "Nadhani maendeleo makubwa yanafanyika Gaza." Akihusisha matumaini yake kuhusu na hatua ya nyingine ya kusitishwa vita vya Siku 12 kati ya Israel na Palestina.
Soma zaidi:Mkutano wa kilele wa NATO waingia siku ya pili na ya mwisho
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anakabiliwa na wito unaoongezeka kutoka kwa wanasiasa wa upinzani, jamaa wa mateka wanaozuiliwa Gaza na hata wanachama wa muungano wake unaotawala kusitisha mapigano haya ya Israel na Hamas.
Chanzo: AFP