Zaidi ya Wapalestina 90 wauawa Ukanda wa Gaza
3 Julai 2025Takwimu hizo zilizosasishwa zimetolewa Alhamisi na hospitali kadhaa pamoja na Wizara ya Afya ya ukanda huo chini ya kundi la Hamas. Kulingana na mamlaka hizo, watu watano kati ya waliouwawa, walishambuliwa nje ya maeneo yanayohusishwa na taasisi mpya ya kiutu ya Kimarekani ya kutoa msaada wa chakula inayoungwa mkono na Israel. Watu wengine 40 waliuwawa katika maeneo mengine wakisubiri misaada.
Wizara ya mambo ya ndani ya Gaza chini ya kundi la Hamas imetahadharisha wakaazi wa Gaza wasitoe ushirikiano kwa taasisi hiyo ikisema mashambulizi karibu na mahali inapogawa chakula yanahatarisha maisha ya Wapalestina wanaokabiliwa na njaa kali.
Kuhusu hali hiyo inayoendelea Ukanda wa Gaza, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Francesca Albanese, ametoa ripoti mbele ya baraza la u salama la umoja huo akiishutumu zaidi Israel. Zaidi alisema kuwa, " Israel imetumia mauaji ya kimbari kama fursa ya kujaribu silaha mpya na mifumo yao ya uchunguzi, ndege za rubani na teknolojia nyingine kuwaangamiza watu bila kusita."
Israel yakanusha kufanya mauaji ya kimbari
Hata hivyo Israel imeikosoa ripoti ya Albanese na kusema "haina msingi wa kisheria, na kwamba hayo ni matumizi mabaya ya wadhifa wake.
Wakati hayo yakiendelea chanzo kilicho karibu na wanamgambo wa kundi la Hamas la Palestina kimesema kundi hilo linataka kuhakikishiwa kuwa pendekezo jipya la Marekani la kusitisha vita litapeleka vita kukoma Ukanda wa Gaza.
Vyanzo vingine vya kiusalama vya Misri vikisema wasuluhishi kutoka nchini humo na Qatar wanafanya juhudi za kupata hakikisho la kimataifa kuwa mazungumzo ya kukomesha vita yataendelea, hiyo ikiwa ni njia ya kuishawishi Hamas ikubaliane na mpango wa Marekani wa kusimamisha mapigano kwa miezi miwili.
Awali, katika kile kinachoonekana kama jibu la kwanza la Hamas tangu Rais wa Marekani Donald Trump alipotangaza kile alichokiita mpango wa kusitisha mapigano, kundi hilo lilisema bado linaendelea kuyafikiria mapendekezo mapya yaliyomo kwenye mpango huo.