Mashambulizi ya Israel yaendelea Gaza
27 Mei 2025Katika eneo la Mji wa Gaza pekee, mashambulizi ya anga yaliwauwa Wapalestina 30, wakiwemo wanawake na watoto waliokuwa wamejihifadhi kwenye jengo moja la skuli.
Picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha miili iliyoteketea vibaya kwa moto ikifukuliwa kutoka kwenye vifusi vya jengo hilo.
Jeshi la Israel limekiri kulishambulia jengo hilo, likiendeleza madai yake kwamba jengo hilo lilikuwa likitumika kama kituo cha kupangia mashambulizi na wanamgambo wa Hamas na Islamic Jihad.
Soma zaidi: Merz asema matendo ya Israel Gaza 'hayana tena uhalali'
Lakini Farah Nussair, mmoja wa manusura wa mashambulizi hayo, amesema kuwa waliokuwamo kwenye jengo hilo walikuwa watu waliochoka kwa njaa na kiu pekee.
"Tulikimbilia kusini, wakatupiga mabomu. Tukarejea kaskazini, wakatupiga mabomu. Tukaja kwenye skuli. Hakuna palipo salama, si skuli, si hospitali, si popote." Alisema mwanamke huyo akiwa na mtoto mchanga mapajani mwake.
Jeshi la Israel ambalo linadai kuwa lilitumia silaha zinazolenga kwa umakini wa hali ya juu, vifaa vya uchunguzi na hatua nyengine kadhaa kuepuka madhara kwa raia, halikutowa, hata hivyo, ushahidi wowote unaothibitisha kuwa jengo hilo lilikuwa likitumiwa na wanamgambo.
Mashambulizi mengine kwenye kitongoji cha Jabalia yaliuawa watu 15, kwa mujibu wa maafisa wa afya.
Ujerumani yasema hali ya Gaza haikubaliki
Hayo yakijiri, Ujerumani - ambayo kwa kawaida ni muungaji mkono wa Israel kijeshi, kifedha na kisiasa - imekosowa vikali kile kinachoendelea sasa kwenye Ukanda wa Gaza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johan Wadephul, alisema akiwa ziarani nchini Uhispania hapo jana kwamba hata nchi yake haiioni hali ya Gaza kuwa yenye kukubalika na kuvumilika tena.
Soma zaidi: Ujerumani yaikosoa Israel kwa vita vyake huko Gaza
Hata hivyo, Wadephul, ambaye alikuwa na mwenzake wa Uhispania, José Manuel Albares, alisisitiza kwamba usalama wa Israel ni "sababu ya kitaifa" kwa Ujerumani - msamiati unaotumika kuelezea wajibu wa kihistoria wa Ujerumani kufuatia jukumu lake kwenye mauaji ya maangamizi dhidi ya Mayahudi, Holocaust.
Kwa hilo, waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, alithibitisha utayari wa nchi yake kuendelea kuipa silaha Israel, ingawa hapo hapo alikiri kuwa hali ya kibinaadamu kwenye Ukanda wa Gaza inazusha kizungumkuti kikubwa cha kimaadili na kisiasa kwa nchi yake.
Uhispania inaongoza kampeni ya kimataifa ikitaka Israel iwekewe vikwazo vya silaha ili kurejesha amani kwenye eneo la Mashariki ya Kati.