Mashambulizi ya Israel yawauwa zaidi ya watu 30 Gaza
2 Septemba 2025Msemaji wa Shirika la Kuwatetea raia Ukanda wa Gaza Mahmud Bassal, amesema shambulio moja lililenga jengo linalotumiwa kama makazi ya watu na kuwauwa watu 10 kwenye jiji la Gaza. Shambulio jingine limewauwa watu watatu katika mji huo huo.
Mashambulizi mengine nje ya mji huo yameshuhudiwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabaliya ambapo majengo yameharibiwa vibaya. Israel yenyewe inasema imekuwa ikiwalenga wanamgambo pekee na inalinyooshea kidole cha lawama kundi la wanamgambo wa Hamas kwa madhara yanayowapata raia.
Hayo yanaendelea wakati Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Israel HaMoked likiripoti kuwa nchi hiyo inawashikilia Wapalestina 11,040 katika magereza nchini humo. Shirika hilo lisilo la Kiserikali linalokusanya taarifa kutoka kwa mamlaka ya magereza ya Israel linaitaja idadi hiyo kuwa ya juu zaidi kuwa ya Kihistoria.
Ubelgiji yapanga kuitambua Palestina kama taifa
Katika hatua nyingine, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Ubelgiji Maxime Prévot amesema mapema Jumanne kuwa nchi yake itaitambua Palestina kama taifa huru katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baadaye mwezi huu kwa masharti.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, Prevot amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya serikali ya Israel, na dhidi ya vitendo vyovyote vya chuki dhidi ya Wayahudi. Ameongeza pia kuwa vitendo vyovyote vya kutukuza ugaidi kutoka kwa wafuasi wa kundi la Hamas vitachukuliwa hatua.
Aidha, Waziri Mkuu huyo wa Ubelgiji amesema nchi yake imefikia uamuzi huo kutokana na janga la kiutu linaloshuhudiwa Palestina hasa Ukanda wa Gaza, pamoja na ukatili wa Israel kwa kukiuka sheria ya kimataifa.
Amesema hatua ya Ubelgiji hailengi kuwawekea vikwazo watu wa Israel bali inakusudia kuhakikisha kuwa serikali yao inaheshimu sheria ya kimataifa na haki za binadamu.