Mashambulizi ya Israel leo yaua watu 25 huko Gaza
8 Aprili 2025Madaktari katika ukanda wa Gaza wamesema leo kwamba mashambulizi ya anga ya Israel yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo Jumanne yamewaua watu 25 wakiwemo watoto wanane na wanawake wanne.
Israel kwa upande wake imesema imefanya mashambulizi hayo ikiwalenga wapiganaji wa Hamas na kulilaumu kundi hilo kwa mauaji ya raia hao kwa madai kwamba kundi hilo linafanya operesheni zake katika maeneo ya watu wengi.
Soma zaidi: China: Tutapambana hadi mwisho dhidi ya ushuru wa Marekani
Israel imeendelea na mashambulizi yake huko Gaza baada ya kuusambaratisha mpango wa usitishaji wa mapigano mwezi uliopita na kusitisha huduma muhimu kama chakula,mafuta na misaada mingine ya kiutu kuingia kwenye ukanda huo, hatua ambayo vikundi vya haki za kibinadamu vinasema ni uhalifu wa kivita.
Mpaka sasa vita vya Israeli huko Gaza vimeua zaidi ya watu 50,000 kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza iliyo chini ya Hamas na Israel imeapa kwamba itaendeleza mapambano hadi pale Hamas itakapowaachilia mateka wake waliosalia.