Mashambulizi ya Israel huko Gaza yawaua zaidi ya watu 65
14 Mei 2025Takriban watoto 22 wameuawa katika ukanda wa Gaza jana Jumanne na usiku wa kuamkia leo Jumatano katika mfululizo wa mashambulizi ya Israel kwenye eneo la kaskazini mwa Gaza, hayo ni kwa mujibu wa hospitali katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa hospitali ya mji mdogo wa Jabaliya ni kwamba mashambulizi hayo yaliyofanywa siku moja baada ya kundi la wanamgambo la Hamas kumwachilia mateka wa Marekani tayari yamewaua zaidi watu 65 kwa ujumla.
Soma zaidi:Israel yasema imeishambulia hospitali Ukanda wa Gaza
Jeshi la Israel limekataa kutoa maoni kuhusu mashambulizi hayo ingawa limewaonya wakaazi wa eneo la Jabaliya kuyahama makazi yao likidai kwamba eneo hilo ni ngome ya Hamas na linatumika kuandaa mashambulizi.
Hapo jana, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alisema hata kama Hamas ikiwaachilia mateka wake ambao bado inawashikilia, Israel itaendeleza mashambulizi huko Gaza ili kuwatokomeza wanamgambo wa Hamas.