Mashambulizi ya angani ya Israel yauwa zaidi ya 100 Gaza
18 Mei 2025Hayo yamesemwa na maafisa wa afya wa eneo hilo wakati wapatanishi wakiendelea na duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas. Hakujatolewa kauli kutoka kwa jeshi la Israel, ambalo limepanua mashambulizi yake kwenye eneo hilo, na kuua mamia ya watu tangu Alhamisi, katika maandalizi ya mashambulizi mapya ya ardhini katika maeneo ya Gaza. Msemaji wa wizara ya afya inayoongozwa na Hamas huko Gaza Khalil Al-Deqran ameiambia Reuters kuwa mashambulizi hayo ya usiku kucha yameziangamiza kabisa familia nyingi za eneo hilo.
Soma pia: Umoja wa Mataifa watoa wito wa usitishwaji vita Gaza
Israel imezuia uingizaji wa vifaa vya matibabu, chakula na mafuta huko Gaza tangu mwanzoni mwa mwezi Machi ili kujaribu kuishinikiza Hamas kuwaachia huru mateka wa Israel. Aidha imeiidhinisha mipango ambayo inaweza kuhusisha kutwaa ukanda mzima wa Gaza na kudhibiti shughuli za misaada.
Hamas inasema itawaachia tu mateka kama Israel itasitisha mashambulizi yake. Wapatanishi wa Misri na Qatar, wakiungwa mkono na Marekani, walianza duru mpya ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili jana Jumamosi. Duru hata hivyo zinasema hakuna hatua zilizopigwa mpaka sasa kwenye mazungumzo hayo.