Kongo: Mashambulizi ya ADF yasababisha mauaji ya raia
10 Machi 2025Siku ya Jumamosi kundi la ADF lilikishambulia kijiji cha Ngohi Vuyinga katika eneo la Lubero, jimbo la Kivu Kaskazini, watu 9 waliuwawa na wengine wengi kupoteza makaazi yao baada ya nyumba zao kuchomwa moto, hii ikiwa ni kulingana na Samuel Kagheni moja ya viongozi wa mashirika ya kiraia katika kijiji hicho.
Kagheni alisema ADF iliwashambulia wakaazi hao kwa mapanga na marungu wakati walipokuwa mashambani mwao huku akisisitiza kuwa idadi ya waliouwawa huenda ikapanda kufuatia watu wengi kutojulikana walipo.
Mashambulizi ya ADF yasababisha vifo vya watu 12 Kongo
Eneo la Mashariki mwa Kongo linapitia miongo kadhaa ya ghasia za makundi yenye silaha. Zaidi ya vikundi 120 vinapigania ushawishi, ardhi na rasilimali muhimu za madini. Miongoni mwa makundi hayo ni M23 wanaoungwa mkono na Rwanda ambao hivi karibuni, waliviteka vijiji viwili muhimu vya Goma na Bukavu. Ghasia nchini humo zimesababisha karibu watu milioni 7 kuyakimbia makazi yao na kuifanya hali hiyo kuwa moja ya migogoro mibaya ya kibinaadamu kuwahi kushuhudiwa.
Wakaazi wa kijiji cha Ngohi Vuyinga wamesema mashambulizi ya waasi yanayoendelea katika sehemu mbali mbali za Kongo yanawapa wasiwasi wa usalama wao huku wakiishutumu serikali kwa kutochukua hatua za kutosha, kuwalinda kutiokana na ghasia hizo.
M23 inalenga mahospsitali na miundo mbinu katika mashambulizi yao
Huku hayo yakiarifiwa Shirila la Umoja wa Mataifa linaloratibu misaada ya kiutu OCHA limesema mashambulizi mengine yanayofanywa na kundi jengine la waasi la M23 yamelenga mahospitali na miundo mbinu ya raia mashariki mwa Kongo. Shirika hilo limesema kati ya Machi mosi na Machi 3 hospitali kadhaa zililengwa katika vita vya kongo vinavyozidi kupamba moto hali inayolazimisha baadhi ya hospitali na shule kufungwa.
UNHCR: Watu 800,000 waikimbia Kongo kutokana na mzozo
Hali inavyozidi kuwa mbaya, serikali ya Kongo nayo inaendelea kutoa lawama za moja kwa moja kwa jirani yake Rwanda inayoamini inawaunga mkono waasi wa M23 walioteka eneo lililo na utajiri mkubwa wa madini nchini Kongo. Hata hivyo Rwanda imeendele kukanusha hilo ikisema nayo pia inakabiliwa na vitisho vya usalama kutoka kwa kundi la waasi wanaopigana nchini Kongo.
Siku ya Jumapili wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema iko tayari kuwa na makubaliano ya uchimbaji madini na Kongo baada ya seneta mmoja wa Kongo kuwasiliana na Marekani kutaka makubaliano hayo yafanyike ili DRC ipate makubaliano ya kiusalama. Kongo ina utajiri mkubwa wa madini ya Cobalt, lithium na Urani
Chanzo: ap/reuters/afp